DCI ajivunia kwa kupungua uhalifu

09Nov 2019
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
DCI ajivunia kwa kupungua uhalifu

MKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robart Boaz, amesema katika miaka minne ya serikali ya awamu ya tano, Jeshi la Polisi limefanikiwa kupunguza makosa makubwa ya uhalifu nchini.

MKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robart Boaz, picha mtandao

Akizungumza na Nipashe juzi kuhusu mafanikio ya jeshi hilo katika miaka minne ya serikali ya awamu ya tano, DCI Boaz alisema jeshi hilo pia limeongeza uwajibikaji.

"Utakumbuka wakati Rais John Magufuli anaingia madarakani, alipohutubia Bunge (Novemba 20, 2015) alitupa maneno mengi ambayo yalikuwa ni changamoto kwetu.

“Rais alisema angependa kuona uhalifu, hasa ujambazi, unatokomezwa, hakupenda kuona tena wananchi wanakuwa wanyonge na wenye hofu kwa sababu ya uhalifu.

"Ni kweli hakuna maendeleo pasipokuwa na amani, na sisi kwa kutambua hilo na kuzingatia kazi tuliyopewa na Rais, tulijipanga kuhakikisha tunafanya kazi kwa bidii kupambana na uhalifu huo," Boaz alisema.

Alieleza kuwa katika kipindi hicho cha miaka minne, Jeshi la Polisi limefaulu kudhibiti makosa makubwa ya uhalifu yaliyokuwa yanasumbua nchini, yakiwamo mauaji, ujambazi katika taasisi za fedha na uhalifu mwingine wa kutumia silaha.

Alibainisha kuwa kabla ya utawala wa serikali ya awamu ya tano, kuanzia mwaka 2011 hadi 2015, makosa makubwa ya uhalifu yalikuwa 327,935 wakati katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya tano, makosa hayo yamepungua na kuwa na makosa 246,317.

Aliongeza kuwa mwaka 2011 hadi 2015, matukio ya mauaji yalikuwa 14,960 na katika miaka minne ya serikali ya awamu ya tano, yamepungua hadi kufikia 1,097.

Kwa upande wa makosa ya usalama barabarani, alisema makosa makubwa katika eneo hilo kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2011 hadi 2015 yalikuwa 73,871 na miaka minne ya serikali ya awamu ya tano yamepungua na kuwa na makosa 22,621.

Boaz alisema makosa ya unyang`anyi wa kutumia silaha, mwaka 2011 hadi 2015 yalikuwa 4,515 na miaka minne ya utawala wa serikali ya awamu ya tano yamepungua hadi kufikia 2,070.

“Kwa takwimu hizo tu, unaweza kuona kwamba amani imezidi kuongezeka katika kipindi hiki cha miaka minne ya serikali ya awamu ya tano.

"Haya ni mafanikio makubwa kwa maana kwamba wananchi wako huru zaidi kufanya shughuli zao kwa amani na utulivu, na sisi tunamshukuru sana Rais John Magufuli, amesaidia kutuongeza nguvu zaidi kwa kutujengea mazingira mazuri na ari ya kufanya kazi kwa bidii.

“Tutahakikisha kwamba matukio haya ya uhalifu yanazidi kupungua ili wananchi waendelee kuendesha shughuli zao za kiuchumi kwa kujiamini zaidi pasi na hofu ya kukumbana na wahalifu.

"Rais ametuwezesha kupata vitendea kazi vingi na vyenye ubora, makazi mazuri ya askari. Sasa, mfanyakazi akilala kwenye nyumba nzuri na familia yake iko mahali pazuri, ni lazima afanye kazi nzuri zaidi na ndiyo maana hata nidhamu yao kwa sasa imeongezeka sana.

“Hatusemi kwamba makosa haya yameisha kabisa, lakini sehemu kubwa ya askari, nidhamu yao imeimarika sana na hata kwa wachache ambao wanakosea, tumekuwa tukichukua hatua haraka sana kuwapeleka mahakamani na wengine kuwafukuza kazi kabisa," alisema.

Boaz alisema jeshi hilo liko katika utekelezaji wa mpango wake wa kupeleka askari kuanzia kwenye ngazi ya kata nchini.
“Kila kata itakuwa na askari wake ambaye atakuwa anaiongoza na lengo ni kutaka kuimarisha ulinzi kuanzia katika maeneo wanakoishi wananchi, na pia itasaidia zaidi kujua aina ya wananchi wanaoishi katika kata husika na kufichua zaidi wahalifu," alisema.

Habari Kubwa