DED SINTOO: Tunawapa mikopo ili mchangie pato la taifa

15Jun 2019
Godfrey Mushi
Nipashe
DED SINTOO: Tunawapa mikopo ili mchangie pato la taifa

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Yohana Sintoo amesema mikopo hiyo ni mahususi kwa ajili ya kuinua kipato cha kaya, lakini pia kuwaongezea wananchi uwezo wa kuchangia pato la taifa kwa kulipa kodi ili kuiwezesha serikali kutoa huduma bora kwao.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Yohana Sintoo (katikati) akikabidhi hundi ya mfano kwa mmoja wa wajasiriamali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Yohana Sintoo amesema mikopo hiyo ni mahususi kwa ajili ya kuinua kipato cha kaya, lakini pia kuwaongezea wananchi uwezo wa kuchangia pato la taifa kwa kulipa kodi ili kuiwezesha serikali kutoa huduma bora kwao.

Sintoo alikuwa akikabidhi jana, hundi za mfano kwa vikundi 16 vya wanawake, vijana na walemavu. Mkurugenzi huyo alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.

Sintoo alisema kuwa mikopo hiyo ina thamani ya Sh. milioni 84,349,528.

Kwa mujibu wa Sintoo, mgao huo unahusisha vikundi 16 vya wajasiriamali ambao kati yao vikundi vya wanawake ni 11, vijana vitatu na vikundi viwili vya watu wenye ulemavu.

Sintoo ameeleza zaidi: "Tunakabidhi mikopo hii kwa wajasiriamali kama sehemu ya halmashauri kuinua uchumi wa wananchi wake. Mnatakiwa kutumia fedha hizi kwenye miradi ya kiuchumi mnayoiendesha ili kujiongezea kipato na kuchangia pato la taifa."

Baada ya makabidhiano hayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Hai (DAS), Upendo Wella akitoa nasaha zake katika hafla hiyo, amewasisitiza wanavikundi hao kuwekeza fedha hizo kwenye miradi yenye tija hasa ikizingatiwa elimu waliyopatiwa ya matumizi sahihi ya fedha za mikopo.

Halmashauri ya Wilaya ya Hai imetoa mikopo hiyo kutokana na asilimia 10 ya makusanyo ya mapato ya ndani kwa awamu ya pili kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

Habari Kubwa