Dereva auawa jaribio kumpora askari silaha

20Oct 2021
Said Hamdani
Lindi
Nipashe
Dereva auawa jaribio kumpora askari silaha

MKAZI wa Dar es Salaam, Ibrahim Said, mwenye umri kati ya miaka 30, amefariki dunia kwa madai ya kujaribu kupora silaha kutoka kwa askari polisi waliokuwa zamu katika kizuizi eneo la viwanda vidogo (SIDO) mjini hapo.

Said ambaye ni dereva wa kampuni ya Dangote inayozalisha saruji mkoani Mtwara, alikutwa na umauti usiku wa Oktoba 17, mwaka huu, saa 5:30 katika barabara kuu ya Kibiti - Lindi-Mingoyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Kamishna Msaidizi (ACP) Mtatiro Kitinkwi, alisema dereva huyo alikutwa na mauti kwa madai ya kutotii amri ya kusimama alipotakiwa na askari waliokuwa zamu katika kizuizi hicho.

Alisema dereva huyo akiwa na mwenzake (hakumtaja jina), alikuwa anaendesha lori la kampuni ya Dangote lenye namba za usajili T 992 DJZ lenye tela T 693 DKA.

Kamanda Kitinkwi alisema dereva hiuyo na mwenzake walipofika eneo hilo, askari waliwasimamisha kwa ajili ya ukaguzi lakini akakataa kutii amri.

“Huyu dereva aliposimamishwa na askari wetu waliokuwa zamu eneo lile, alikataa na badala yake akawa anampelekea gari kwa lengo la kutaka kumgonga,” alisema Kitinkwi.

Kitendo cha askari kulikwepa lori hilo, alisema sehemu ya tela iligonga barabara na kwenda porini na kugonga mti, hivyo kusababisha hasara ya chombo husika kikiwemo kioo cha mbele.

Alisema baada ya lori hilo kugonga mti, Said alitelemka na kwenda kumvamia askari mwingine aliyekuwa na bunduki na kuanza kumchoma kisu sehemu mbalimbali za mwili wake kwa lengo la kutaka kumpora.

Kamanda Kitinkwi alisema kabla ya dereva huyo hajafanikiwa kuipora bunduki kutoka kwa askari huyo, wenzake aliokuwa nao zamu walimdhibiti na kupiga risasi hivyo kufariki dunia.

Alisema katika tukio hilo, ofisa mmoja na askari wawili waliumizwa na kupelekwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa ya sokoine kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Pia alisema wanaendelea na uchunguzi kubaini iwapo Said alikuwa dereva halali wa kampuni hiyo.

Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni ACP Andrew Ngassa aliyelazwa wodi namba sita, Konstebo David Mbunda na Konstabo Denis Somanga, ambao wametibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani.

Kaimu Mganga Mfawidhi Hospitali ya Sokoine, Dk, Dismas Mjarufu, alithibitisha  kupokea majeruhi watatu ambao ni askari Polisi wakiwa na majeraha maeneo mbalimbali ya miili  na mwili wa mtu mmoja aliyefariki dunia.

“Mpaka sasa yuko askari mmoja amelazwa chumba namba sita na wawili wametibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani,” alisema Dk. Mjarufu.

Dk. Mjarufu alisema majeruhi hao wamepata majeraha maeneo ya shingoni, mabegani na mikononi na kwamba hali zao zinaendelea vizuri.

Habari Kubwa