Dereva gari lililoua wanafunzi 5 Songea atiwa mbaroni Dar

17Feb 2020
Gideon Mwakanosya
Ruvuma
Nipashe
Dereva gari lililoua wanafunzi 5 Songea atiwa mbaroni Dar

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, linamshikilia dereva wa gari lililosababisha vifo vya wanafunzi watano wa Shule ya Msingi Ndelenyuma, Wilaya ya Madaba na kujeruhi mmoja.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Simon Maigwa, picha mtandao

Deveva huyo Salum Mohamed, alikamatiwa Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, alikokimbilia baada ya tukio hilo kutokea wiki iliyopita.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Simon Maigwa, alisema dereva huyo alikamatwa mchana wa Februari 15, mwaka huu kwa ushirikiano kati ya polisi na jamii.

Aidha, alisema askari kutoka Songea ametumwa kwenda kumfuata na kumleta Ruvuma kwa ajili ya kuhojiwa na hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yake.

Ajali hiyo ilitoke Februari 12, majira ya saa nane mchana katika kijiji cha Ndelenyuma kwa gari lenye namba za usajili T 443 AQT aina ya Toyota Land Cruiser mali ya kampuni ya CAMUST likitoka Songea kuelekea Njombe kuacha njia na kuwagonga wanafunzi sita wenye umri wa miaka 10 hadi 13 wa darasa la pili hadi nne.

Baada ya kuwagonga gari hiyo ilipinduka na dereva alitoka na kutorokea kusikojulikana.

Mwanafunzi Hilda Kilasi (12) mwanafunzi wa darasa la nne, anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Mkoa Songea na hali yake inaendelea vizuri.

Kwa mujibu wa Kamanda Maigwa, chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva ambaye inadaiwa hakujali hali ya mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha kwenye eneo la kijiji hicho na utelezi kwenye barabara hiyo hatimaye gari lilimshinda na kuwagonga wanafunzi hao ambao walikuwa pembeni mwa barabara wakitembea kwa miguu kuelekea nyumbani wakitokea shuleni na kudondokea mtaroni ambapo watatu walisombwa na maji na miili yao kuokotwa takribani mita 100 kutoka eneo la tukio na wengine wawili walikutwa mtaroni jirani na eneo la ajali.

Habari Kubwa