Dereva taksi kesi ya Mo aendelea kusota, wengine wasakwa

16Sep 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Dereva taksi kesi ya Mo aendelea kusota, wengine wasakwa

UPANDE wa Jamhuri katika kesi inayomkabili dereva taksi mkazi wa Tegeta, Mousa Twaleb (46) ya uhujumu uchumi ikiwamo kusaidia kutendeka uhalifu, kutakatisha Sh. Milioni 8 na kumteka Mohamed Dewji maarufu kama Mo-

-umedai kuwa bado unaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine wanne kwa ajili ya kuwaunganisha katika kesi hiyo.

Kesi hiyo ilitajwa leo Septemba 16,2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Wakili wa Serikali Mwandamizi,  Wankyo Simon  alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba bado upande wa Jamhuri unaendelea na juhudi za kuwatafuta watuhumiwa wengine.

Alidai kuwa upande wa Jamhuri unaomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu alisema kesi hiyo itatajwa tena Septemba 30,mwaka huu na mshtakiwa ataendelea kukaa mahabusu.

Mapema mahakamani hapo, Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi alidai kuwa kati ya Mei Mosi na Oktoba 10, 2018 mahali tofauti jijini Dar es Salaam na jijini Johannesburg nchini Afrika ya Kusini, kwa makusudi alisaidia utendaji makosa ya jinai kwa nia ya kujipatia fedha.

Habari Kubwa