Dhamana ya Lema 'leo' heri jana

05Jan 2017
John Ngunge
ARUSHA
Nipashe
Dhamana ya Lema 'leo' heri jana

SARAKASI za kisheria zimeendelea katika shauri la maombi ya dhamana ya Godbless Lema, baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha notisi ya kupinga rufani ya Mbunge wa Arusha Mjini huyo isisikilizwe na Mahakama Kuu, imeelezwa.

Godbless Lema (Chadema), akiwapungia mkono wafuasi wa chama hicho, alipokuwa akitoka kusikiliza rufani yake.

Kufuatia notisi hiyo iliyosajiliwa Ijumaa iliyopita katika masjala ya Mahakama ya Rufani Arusha, shauri la dhamana ya Lema sasa litatinga Mahakama ya Rufani katika siku itakayopangwa.

Lema ambaye ni Mbunge wa Chadema amekuwa mahabusu tangu alipokamatwa na polisi mjini Dodoma Novemba 2, mwaka jana, akituhumiwa kufanya uchochezi dhidi ya serikali.

Jaji Salma Magimbi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, ambaye alitarajiwa kusoma uamuzi wa ama kumpa Lema dhamana au la jana, alisema hawezi tena kuamua suala hilo kwa sababu ya notisi hiyo ya Jamhuri.

Awali Jamhuri ilikuwa imewasilisha Mahakama Kuu kanda ya Arusha notisi ya kupinga ombi la dhamana lililowasilishwa na mawakili wa Lema.

Mawakili wa Lema walikuwa wakipinga ombi la mawakili wa Serikali walilolitoa mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Desderi Kamugisha, Novemba 11 mwaka jana.

Katika ombi hilo, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Paul Kadushi, aliwasilisha notisi ya kukata rufani Mahakama Kuu kupinga Lema kupewa dhamana, ombi ambalo alilitamka muda mfupi kabla ya Hakimu Kamugisha kutoa masharti ya dhamana.

Rufani hiyo ndiyo iliyotarajiwa kutolewa uamuzi jana, lakini Jaji Magimbi alisema hawezi kufanya hivyo kwa sababu upande wa
Jamhuri umeshawasilisha notisi ya kupinga rufani yao isisikilizwe.

Alisema shauri hilo sasa litasikilizwa Mahakama ya Rufani.

Desemba 28, mwaka jana, Mahakama Kuu iliutaka upande wa Jamhuri kuwasilisha hoja za kupinga dhamana ndani ya siku moja ili mawakili wa Lema waweze kujibu hoja hizo Desemba 30.

Jumatatu iliyopita ilipangwa kuwa siku ya kutoa hoja za ziada kwa pande zote mbili na mahakama hiyo ingetoa uamuzi kuhusu suala hilo jana.

Jana upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili Mwandamizi Innocent Njau, wakati upande wa Lema uliwakilishwa na mawakili Peter Kibatala, Adam Jabir, Sheck Mfinanga, Faraji Mangula na John Mallya.

UHUNI WA KISHERIA
Akizungumza nje ya mahakama, Mallya alisema mawakili wa serikali wamefanya "uhuni wa kisheria" wa kupinga katika Mahakama ya Rufani ombi la rufani yao wenyewe lisisikilizwe.

Alisema utaratibu uliotumika haupo kisheria na wamejipanga kuipinga notisi hiyo Mahakama ya Rufani.

“Mahakama ya Rufani ndiyo ya mwisho, hawawezi (mawakili wa serikali) kuendelea kukwepa tena. Tutakutana huko,” alisema.
Wakili wa Serikali Njau, hakutaka kuzungumza na wanahabari wala kuwasikiliza alipoombwa kutoa ufafanuzi zaidi.

Novemba mwaka jana hakimu Kamugisha wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha aliamuru dhamana ya Lema ipo wazi, lakini upande wa Jamhuri ulitoa notisi ya kukata rufani Mahakama Kuu kumpinga.

Mawakili wa serikali wakiongozwa na Mwanasheria Mwandamizi, Kadushi, walipinga Lema kupewa dhamana katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi kwa madai kuwa amefanya kosa aliloshtakiwa nalo akiwa amepewa dhamana na mahakama hiyo katika shtaka lingine kama hilo.

Pia walidai kuwa Lema kupewa dhamana kulikuwa ni hatari ya usalama wa maisha yake.

Akitupilia mbali hoja hizo, Hakimu Kamugisha alisema mahakama haitoi dhamana kama hisani, bali ni haki ya msingi ya mtuhumiwa kama ilivyoainishwa katika Katiba ya nchi na sheria mbalimbali.

Alisema iwapo mtuhumiwa ananyimwa dhamana, sheria inatakiwa kutamka bayana.

Habari Kubwa