DHL yatoa msaada wa boti kwa ajili ya uvuvi, ulinzi Ziwa Tanganyika

10Apr 2022
Faustine Feliciane
Nipashe Jumapili
DHL yatoa msaada wa boti kwa ajili ya uvuvi, ulinzi Ziwa Tanganyika

KAMPUNI ya Huduma ya Usambazaji Kimataifa ya DHL imetoa msaada wa boti ya kisasa kwa serikali kwa ajili ya kuimarisha ulinzi kwenye Ziwa Tanganyika.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika mkoani Kigoma, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, alisema msaada huo utaenda kuchochea Uvuvi na utunzaji wa ziwa hilo lenye manufaa makubwa kwa wananchi wa Kigoma na maeneo ya jirani.

“Tunatambua kwamba sekta ya uvuvi imebadilika na kuwa shughuli muhimu ya kiuchumi badala ya kuwa suala la mazingira au viumbe hai na hivyo ni lazima tuilinde na kulinda maji yetu, msaada huu wa boti umekuja katika kipindi muhimu wakati huu wa mapinduzi ya uchumi wa bluu na kuunga juhudi za Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan  katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.”  alisema Waziri Ndaki.

Alisema kuwa boti hiyo ya kisasa itatumika kwa namna ilivyopangwa ikiwa pia kuongeza nguvu ya ulinzi wa ziwa hilo. 

Mkurugenzi Mtendaji wa DHL Express Tanzania, Paul Makolosi, alisema mchango wao wa boti ya ulinzi katika sekta ya uvuvi mkoani Kigoma utasaidia wavuvi kufanya kazi zao kwa ufanisi katika eneo la Ziwa Tanganyika ikiwemo kuvua samaki kwa usalama zaidi na kufikia malengo waliyojiwekea.

“Katika mioyo yetu tumekuwa na utaratibu wa kuwaunganisha watu kwa vitendo, DHL imekuwa ikifanya mambo mbalimbali kwa ajili ya kusaidia maisha ya wengi, sisi kama kampuni tunafanya kile ambacho kipo ndani ya uwezo wetu, sio tu kampuni ya kusambaza vifurushi lakini tumekuwa tukisaidia mambo mbalimbali kwa jamii inayotuzunguka,” alisema Makolosi.

Aidha alisema umuhimu wa ziwa hilo kwa wakazi wa Kigoma na maeneo ya jirani umewagusa kutoa msaada huo wa boti kusaidia ulinzi na shughuri nyingine za uvuvi.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa DHL kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, Fatima Sullivan, aliongeza kama kichocheo cha biashara na uwekezaji wenye athari nyingi kwa uchumi mpana wa kijamii na kiuchumi, DHL imeendelea kunufaisha biashara zinazolenga mauzo ya nje nchini Tanzania na huduma za  wakati na sahihi.

“Taarifa za utoaji, ukiangalia zaidi ya mtazamo wa biashara, uwajibikaji wa kampuni ni sehemu muhimu ya mkakati wetu wa ushirika na Kigoma ni mji ambao uko karibu na mioyo yetu nchini Tanzania na ndio sababu ya kutumia rasilimali zetu ili kusaidia jamii kwa njia chanya. 

“Sekta ya uvuvi nchini Tanzania ina mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kuchangia katika ustawi wa kiuchumi na kijamii wa nchi hususani katika usambazaji wa protini za wanyama, kuongeza kipato, ajira, utalii na usalama wa chakula, DHL tutaendelea kusaidia shughuri za kijamii za maendeleo kwa Watanzania.

Habari Kubwa