Ditopile, DMC wametembelea wafungwa Gereza la Kondoa na kutoa futari

25Apr 2021
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe Jumapili
Ditopile, DMC wametembelea wafungwa Gereza la Kondoa na kutoa futari

MBUNGE wa Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile, pamoja na Jumuiya ya Waislamu (DMC) wametembelea Gereza la Wilaya ya Kondoa na kupeleka mahitaji mbalimbali ikiwemo Futari kwa wafungwa na mahabusu wa gereza hilo.

Akizungumza baada ya kukabidhi mahitaji hayo, Mbunge huyo ameahidi kushirikiana na uongozi wa Gereza hilo katika kukamilisha ujenzi wa zahanati inayojengwa ambayo pia itakua msaada mkubwa kwa wananchi wa maeneo jirani.

Ditopile amesema pia amepokea changamoto kutoka kwa Mkuu wa Gereza hilo, Julius Nachunga, ambaye ameomba msaada wa mashine ya kupasulia mawe kwani wanao mradi wa kupasua mawe ambao kama wakipata mashine wataufanya kwa ufanisi zaidi na utawaingizia kipato kikubwa ambacho kitawasaidia kama Gereza katika kujiendesha.

” Mimi kama Mbunge wa Mkoa wa Dodoma na mwanachama wa DMC leo tumefika kuwasilimu wafungwa na mahabusu, pamoja na kuwafariji pia tumewaletea mahitaji mbalimbali ikiwemo futari kama tunavyofahamu huu ni mwezi Mtukufu wa Ramadhan, nguo za aina zote kama kanzu kwa ajili ya kuswalia, taulo za kike kwa ajili ya wafungwa wanawake, tunafanya hivi kwa upendo tukitambua hawa ni ndugu zetu na wanahitaji faraja" amesema Ditopile.

Kama gereza wana miradi yao ikiwemo wa kupasua mawe, lakini hawana vifaa kama Mashine ile ya kupasulia na badala yake wanatumia mikono, nimemuahidi pia Mkuu wa gereza kushirikiana nao tuweze kupata mashine hiyo ili waitumie pia katika kuwaingizia kipato kitakachowasaidia katika mahitaji yao mbalimbali.

Habari Kubwa