Diwani jela miezi 6 uharibifu wa mali

25Oct 2021
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
Diwani jela miezi 6 uharibifu wa mali

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro mkoani hapo, Lucas Lemomo, amehukumiwa jela miezi sita bila kulipa faini kwa kosa la uharibifu wa mali katika Mahakama ya Mwanzo Ngerengere, wilayani Morogoro.

Lemomo ambaye ni Diwani wa Kata ya Matuli, alishtakiwa kwa makosa matatu yote ya uharibifu wa mali kwa kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima na kuharibu mazao.

Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Ngerengere, Godfrey Ng'itu, alieleza juzi wakati akitoa hukumu kuwa Lemomo alikabiliwa na kesi namba 133 ya mwaka 2021 mahakamani hapo na mlalamikaji ni Athuman Abdallah, mkazi wa Mikobora, Kata ya Ngerengere na kesi ya pili namba 122 ya mwaka 2021, mlalamikaji ni Athuman Abdalllah, mkazi wa Visaraka Ngerengere.

Hakimu wa mahakama hiyo alisema baada ya upande wa mshtaka kuthibitisha shtaka pasipo shaka lolote, mshtakiwa katika kesi zote mbili ametiwa hatiani kwa mujibu wa fungu 37(1) kanuni za Mwenendo wa Makosa ya Jinai katika Mahakama ya Mwanzo.

Hakimu Ng'itu alisema hukumu haikuwa na mbadala wa kulipa faini.

Mshtakiwa kwenye kesi ya kwanza amehukumiwa kwenda gerezani miezi sita na baada ya kutoka ametakiwa kulipa fidia ya mazao yaliyoharibiwa na mifugo Sh. 79,000.

Kesi ya pili amehukumiwa kwenda jela miezi sita bila faini na akitoka ametakiwa kulipa fidia ya Sh. 440,000 na kwamba kifungo hicho ni kwa pamoja wakati kesi yake nyingine ya jinai itasomwa hukumu Novemba 3, 2021.

Habari Kubwa