Diwani kortini shtaka la kupokea rushwa mil. 1/-

22May 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Diwani kortini shtaka la kupokea rushwa mil. 1/-

DIWANI wa Kata ya Kijichi Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Elias Mtarawanje (29), amefikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka mawili ikiwamo kushawishi na kupokea rushwa ya Sh. milioni moja kutoka kwa Yusuf Omary.

Mshtakiwa huyo alisomewa mashtaka yake jana katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi, Catherine Madili.

Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mwanakombo Rajabu, alidai kuwa Februari 6, mwaka huu eneo la Mtoni Kijichi, Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam mshtakiwa akiwa Diwani wa Kata ya Kijichi, aliomba rushwa ya Sh. milioni moja kutoka kwa Omary kama kishawishi kwake ili asiweze kuzuia malipo ya fidia ya eneo jambo ambalo amelifanya tofauti na uhusiano wa shughuli za mwajiri wake.

Katika shtaka la pili, inadaiwa kuwa Februari 6, mwaka huu, eneo la tukio Mtoni Kijichi mshtakiwa huyo akiwa diwani kwa njia za rushwa alijipatia Sh. milioni moja kama kishawishi kwake ili asiweze kuzuia malipo ya fidia ya eneo, jambo ambalo amelifanya tofauti na uhusiano wa shughuli za mwajiri wake.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa hauna pingamizi la dhamana, upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba mahakama kupanga tarehe ya kumsomea maelezo ya awali.

Akitoa masharti ya dhamana, Hakimu Madili alimtaka mshtakiwa huyo kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh. 500,000, kila mmoja.

Mshtakiwa huyo ametimiza masharti ya dhamana.

Hakimu alisema mahakama yake itasikiliza maelezo ya awali Juni 3, mwaka huu.

Habari Kubwa