Diwani mwigine Moshi atimka Chadema

16Dec 2017
Godfrey Mushi
Nipashe
Diwani mwigine Moshi atimka Chadema

DIWANI mwingine wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema mkoani Kilimanjaro, amejiengua na kutangaza kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Susan Natai (mwenye miwani) akiwa amevishwa skafu ya CCM baada ya kuhammia chama hicho.

Diwani huyo, Susan Natai wa Kata ya Kashashi, wilayani Siha, amechukua uamuzi huo ikiwa siku moja baada ya Mbunge wa Jimbo hilo, Dk. Godwin Mollel, kutangaza kujivua uanachama wa Chadema hivyo kupoteza ubunge wake.

Tayari Spika wa Bunge, Job Ndugai, amekiri kupokea barua ya mbunge huyo juu ya uamuzi wake huo na ameiandikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuiarifu kuwa jimbo hilo liko wazi. 

Hatua ya kujiuzulu kwa mbunge na diwani huyo, kunaipa CCM nafasi ya kuipoka Chadema uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Siha kutokana na kuwa na madiwani wengi.

Chadema inayounda Halmashauri ya Wilaya ya Siha, hata kabla ya Mbunge huyo na Diwani Susan kubwaga manyanga, pia inaongoza halmashauri tano za wilaya za Hai, Rombo, Moshi Vijijini na Manispaa ya Moshi.

Uchunguzi wa Nipashe unaonyesha, CCM kwa sasa itakuwa na madiwani 13 na Chadema madiwani 12. Kabla ya hapo Chadema iliunda halmashauri hiyo kwa turufu ya madiwani 14, akiwamo Dk. Mollel.

Kwa hesabu hizo, Dk. Mollel na Susan wamefungua njia kwa CCM kuipokonya Chadema halmashauri hiyo kama madiwani wa CCM wataibua hoja ya kumkataa Mwenyekiti wa Halmashauri na kutaka kufanyike uchaguzi.

CCM ina faida ya kujiuzulu kwa madiwani hao wawili ambao ni Mbunge na Diwani hata kama hawatasubiri kura za marudio ya kiti cha ubunge na udiwani ambavyo viko wazi kwa sasa. Jimbo la Siha lina jumla ya Kata 17.

Akizungumza muda mfupi baada ya kupokewa rasmi na kukabidhiwa kadi ya CCM, Dk. Mollel alisema: “Haijalishi mimi nitapanda gari la aina gani, ninachotaka niende nilete keki kwa ajili ya watu wa Siha, hicho ndicho kikubwa.

Tuanze kutafakari safari inayoanza, nataka kuwaambia tumekwenda tumeanzisha kazi, sasa mbio ndiyo zimeanza na ndege ndiyo imeshika kasi. Nilikuwa nazungusha injini na sasa nataka niwaaambie ndege ndiyo imepaa hivyo.”

Aliongeza kuwa: “Hebu tuungane, upande ule nina watu waliomwaga damu kwa ajili yangu. Nina watu waliopigwa kwa ajili yangu, nina watu waliofungwa kwa ajili yangu, ni lazima niwaheshimu, ni lazima niwasikilize na nitakuwa na wiki moja ya kuwasikiliza na nataka kuwaambia hawataniangusha. Kama walimwaga damu kwa ajili yangu hawakumwaga kwa ajili ya chama chochote, walimwaga damu kwa ajili ya Siha na Tanzania.”

Akizungumza baada ya kuwakabidhi kadi na kuwaapisha, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, aliwataka wanachama hao wapya kufanya kazi pamoja kwa kuwa maendeleo ya Siha hayakuletwa na chama kingine zaidi ya CCM.

“Mollel amekataa marupurupu mengi, magari mazuri na diwani amekataa posho kwa sababu serikali ni yetu, halmashauri ni zetu na Rais wetu (Magufuli) amejitahidi kwa kiwango kikubwa kuhakikisha kile tunachokipata kulingana na uchumi wa nchi yetu, analeta kidogo kidogo kulingana na matarajio na mahitaji ya panapohusika.  Wengine waliopotea njia kwa bahati mbaya mlango uko wazi,”alisisitiza Boisafi.

Kuhusu uvumi unaoenezwa kwamba CCM inanunua madiwani na wabunge wa upinzani, Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya alisema anataka aliweke sawa jambo hilo kwa kuwa zimekuwapo fununu mitaani, watu wakisema kila anayerejea CCM amenunuliwa.

 “CCM haiamini katika biashara ya utumwa kwa sababu kununua mtu ni kurejea kwenye biashara ya utumwa. Kwetu sisi utu ndio wenye thamani kuliko kupanga bei ya binadamu. Maana yangu ni hii, hatujamnunua Dk. Godwin (Mollel), hatujamnunua mama Natai. Ni hiari yao na wametafakari wakachukua uamuzi wao wenyewe,” alisema.

ALIKOTOKEA DK. MOLLELMwaka 2014, Dk. Mollel aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM), Wilaya ya Siha, alijiunga na Chadema.

Baadaye mwaka 2015, akateuliwa kugombea ubunge na kumshinda Naibu Waziri wa zamani katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) kwa wakati huo, Aggrey Mwanri aliyekuwa mgombea ubunge wa CCM.

SUSAN NATAIHuyu kabla ya kujiunga na Chadema mwaka 2015, alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Siha. 

Kabla ya kuteuliwa kugombea udiwani na kushinda kiti hicho alikuwa mwiba kwa wapinzani kutokana na uwezo wake wa kujenga hoja na kutetea. 

Habari Kubwa