Diwani wa Masama atatua kero ya maji ya muda mrefu

14Apr 2021
Na Mwandishi Wetu
HAI
Nipashe
Diwani wa Masama atatua kero ya maji ya muda mrefu

ADHA waliyoukwa nayo wananchi wa kitongoji cha Dharau, kijiji cha Mkombozi, kata ya Masama Kusini, wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, imeanza kutatuliwa baada ya kuanza kutekelezwa mradi wa maji safi na salama katika kijiji hicho.

Diwani wa Kata ya Masama Kusini Cedrick Pangani akishiriki shughuli ya uchimbaji wa mtaro wa maji kwenye kitongoji cha Dharau kilichopo Kijiji cha Mkombaji Kata ya Masama Kusini wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza wakati wa zoezi la kuchimba mitaro na kufukia mabomba ya maji kwa ajili mradi huo, Diwani wa Kata ya Masama Kusini Cedrick Pangani alisema kuwa mradi huo ni ahadi aliyowaahidi wananchi hao wakati wa kampeni za Udiwani, Ubunge na Urais, zilizofanyika mwaka jana.

"Moja wapo ya ahadi zangu wakati wa kampeni zangu zilikuwa ni kuhakikisha tunatatua kero ya miaka mingi ya ukosefu wa maji safi na salama kwa wananchi wa kijiji hiki na vile vya jirani", alisema Pangani.

Pangani aliendelea kusema kuwa mradi huo umelenga kutatua kero hiyo ambayo imekuwa changamoto kwa wananchi wa eneo hilo kwa miaka mingi ambapo alitoa wito kwa wananchi wa eneo hilo kuendelea kumpa ushirikiano ili kuharakisha maendeleo ya eneo hilo.

Akiongea katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa kitongoji cha Dharau Onesmo Munishi, aliipongeza Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa utekelezaji wa mradi huo ambao alisema utanufaisha zaidi ya kaya 70 zenye wakazi wapatao 360.

"Ukikamilika, mradi huu ambao taarifa zinaonyesha uekelezaji wake umeshafikia asilimia 80, utatatua kero ya maji ambayo ilikuwa ikiwalazimisha wakazi wa eneo hili kutembea zaidi ya kilomita 5 kila siku kutafuta maji safi na salama, swala lililokuwa likitumia muda wao mwingi ambao wangeweza kuutumia kwa shughuli zingine za kimaendeleo", alisema Pangani.

Mjumbe wa serikali ya kijiji cha Dharau Batholomeo Joseph, alisema mradi huo ni ukombozi kwa wananchi wa eneo hilo akiwemo yeye mwenyewe ambapo alisema katika miaka yake 50 tangu kuzaliwa kwake maji safi na salama alikuwa akiyaona na kuyatumia awapo nje ya kijiji alichozaliwa.

Mkazi wa kijiji hicho Mussa Zuberi, alimpongeza Diwani Pangani kwa kuhamasisha sambamba na kushiriki na wananchi katika kutekeleza mradi huo, ambapo alitoa rai kwa Diwani huyo na serikali kwa ujumla kuelekeza nguvu hizo kwenye miradi mingine kama ile ya barabara ili ziweze kutumika vyema ikiwepo kusafirishia wagonjwa kufuata huduma za afya.

Mkazi mwingine Dorosila Ollotu, alisema mradi huo ni ndoto ambayo imekuwa kweli kutokana na ukweli eneo hilo walikuwa hawajapata huduma ya maji safi na salama tangu uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Habari Kubwa