Dk. Bashiru ataja sababu 5 Magufuli kupeperusha bendera CCM

11Jul 2020
Gwamaka Alipipi
DODOMA
Nipashe
Dk. Bashiru ataja sababu 5 Magufuli kupeperusha bendera CCM

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM), Dk. Bashiru Ally ametaja sababu tano zilizowashawishi wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho kumpendekeza Rais John Magufuli kuwania tena nafasi ya urais.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM), Dk. Bashiru Ally.

Akizungumza na wanachama wa chama hicho katika Mkutano Mkuu uliofanyika jijini hapa, Dk. Bashiru amesema sababu ya kwanza ni Rais Magufuli kukidhi vigezo vinavyohitajita kwa mujibu wa sheria za nchi pamoja na Katiba na kanuni za CCM.

"Kanuni ya 6 ya Kanuni za uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya dola, toleo la mwaka 2019 imetaja sifa za msingi 12 za mwanachama anayefaa kuteuliwa kugombea nafasi ya Rais. Kwa vigezo vyote, ukamilifu wa sifa hizo Dk. Magufuli hauwezi kutiliwa shaka na yeyote" amesema Dk. Bashiru.

Dk. Bashiru ametaja sababu ya pili ni kiwango cha utumishi wake uliotukuka kwa wananchi, Taifa na dunia.

Sababu ya tatu ni mchapakazi hodari, mfuatiliaji makini, mzalendo na mwaminifu kwa nchi yake.

"Rais Magufuli ni mpenda haki na mwenye ujasiri na utashi wa kuongoza mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa, uzembe, uvivu, wizi wa mali ya umma" amesema Dk. Bashiru.

Dk. Bashiru ametaja sababu ya nne ni katika uongozi wake wa miaka mitano ameliongoza Taifa kwa heshima na mafanikio makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa.

Amesema sababu ya tano ni wananchi wengi hususani wasio wanachama wa CCM kuridhishwa na utendaji wake.

Habari Kubwa