Dk. Bashiru awatemea cheche wanasiasa

15May 2019
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Dk. Bashiru awatemea cheche wanasiasa

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amekemea wanasiasa wanaoingilia na kuwadhalilisha watoa huduma za afya wakiwamo  madaktari na wauguzi.

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally.

Dk. Bashiru alieleza kusikitishwa na vitendo hivyo baada ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Sikika, kufanya mazungumzo naye ofisi kwake jijini Dodoma jana.

 

Walifanya mkutano huo kwa ajili ya kujadili uhusiano na mawasiliano kati ya wanasiasa na watoa huduma za afya.

 

Katika mazungumzo hayo, pia walijadili kuhusu bajeti ya afya na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya afya Tanzania.

 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotiwa saini na Rais wa MAT, Dk. Elisha Osati na Mkurugenzi Mtendaji wa Sikika, Irenei Kiria, Dk. Bashiru alisema hakuna mtu anayewatuma wanasiasa kufanya hivyo na kuwataka wadau wote kushirikiana na kuwalinda wataalamu wa afya na kuwakinga dhidi ya udhalilishaji.

"CCM iko tayari kushirikiana na wataalam wa afya kutengeneza mazingira bora ya ushirikiano kati yenu na wanasiasa ili kuwahudumia wananchi ipasavyo," alisema.

 

Katika kuondokana na mgongano huo, Dk. Bashiru aliwataka wadau wa afya kutengeneza mkakati wa kutoa elimu ya namna bora ya mawasiliano kati ya wanasiasa na wataalam wa afya.

 

Pia aliwashauri kuchapisha orodha ya mambo yanayotakiwa na yasiyotakiwa kufanywa na wadau mbalimbali wanapokuwa katika mazingira ya hospitali na kisha kuyasambaza katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

 

Kadhalika, aliwashauri liundwe jukwaa litakalojumuisha wanataaluma wa afya, watafiti kutoka vyuo pamoja na asasi za kiraia ili kusaidia kutafsiri tafiti kwenda kwenye uhalisia, kutoa elimu ya afya kwa wananchi na ushauri wa kisera kwa serikali.

 

Taasisi hizo zilimwomba Dk. Bashiru awasisitize wanasiasa kuwatangazia zaidi wananchi kiasi cha fedha zinazotolewa na serikali kuliko fedha zilizotengwa.

"Hii itasaidia kukuza uelewa na kuzuia migongano kati ya wanasiasa na wanataaluma kwa upande mmoja na kutoa huduma na wananchi kwa upande mwingine," ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilieleza mambo mengine yaliyozungumzia kuwa ni pamoja na mwenendo wa utekelezaji wa bajeti ya afya, sera ya msamaha wa matibabu kwa makundi mbalimbali na umuhimu wa kila Mtanzania kuwa na bima ya afya.

 

"Mazungumzo hayo yaligusia changamoto za rasilimali watu katika utoaji wa huduma za afya, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, majengo na miundombinu," ilisema.

 

Pia MAT na Sikika walieleza kuridhishwa kwao na juhudi zinazoendelea kufanyika katika sekta ya afya ikiwamo uboreshwaji wa huduma za kibingwa na ujenzi wa vituo vya afya.

Habari Kubwa