Dk. Kijaji azifunda taasisi za fedha

26Feb 2016
Moshi Lusonzo
Dar
Nipashe
Dk. Kijaji azifunda taasisi za fedha

SERIKALI imezitaka taasisi za kifedha kuwafikia asilimia 80 ya Watanzania kwa kufungua matawi vijijini.

Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. Ashiatu Kijaji.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. Ashiatu Kijaji, wakati wa uzinduzi wa tawi la benki ya Amana la Mbagala, Dar es Salaam.

Benki hiyo imefikisha matawi saba nchini, ikiwa na wateja 27,000 na amana ya jumla ya Sh. bilioni 160.

Dk. Kijaji alisema pamoja na benki hiyo inayofuata misingi ya Kiislamu kupata mafanikio, inatakiwa kupanua wigo wake hadi vijijini kuhakikisha wananchi wananufaika na mfumo rasmi wa kifedha.

“Wakati wa kampeni tumezunguka nchi nzima. Kule vijijini wakulima na wafugaji wanaweka fedha zao nyumbani kwa kukosa mfumo rasmi wa kibenki. Nendeni huko mkatoe huduma kwa manufaa ya wananchi,” alisema Dk. Kijaji.

Alisema fedha nyingi zilizo nje ya mzunguko rasmi wa kifedha zinatoa mchango mdogo katika kukuza uchumi wa nchi.
Dk. Kijaji alisema hatua ya benki ya Amana kufungua tawi Mbagala imezingatia mambo makuu matatu ikiwamo idadi kubwa ya watu, kasi ya ongezeko la watu na kuwa na viwanda vingi.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Amana, Dk. Muhsin Masoud, alisema katika kipindi cha miaka mitano tangu kuanzishwa kwake, benki imeendelea kuwa taasisi bora inayofuata uadilifu, uaminifu na udhibiti kwa misingi ya Kiislamu.

Alisema katika uendeshaji wake, hakuna utaratibu wa riba, badala yake mteja anapata faida kwa kupewa gawio kutokana na faida inayopatikana katika biashara.

Aliwataka wananchi kutumia tawi hilo kwa ajili ya kutunza fedha zao pamoja na kuchukua mikopo kwa wafanyabiashara wadogo.

Habari Kubwa