Akijinadi mbele ya wananchi na wanachama wa CCM katika mkutano wa kampeni katika kata hiyo jana, Dk. Mabula alisema atafanikisha ujenzi wa jengo la kupumzikia mama na mtoto baada ya kuzaliwa, na kumtaka Mgombea udiwani wa kata hiyo kwa tiketi ya CCM, Samwel Mwita kulichukulia kipaumbele suala hilo pindi atakapoingia kwenye Halmashauri.
Dk Mabula, alisema ujenzi wa jengo hilo utasaidia mama na mtoto kupata huduma hiyo bila shida, na kuwapongeza wananchi wa kata ya Kahama hasa mtaa wa Lukobe kwa kufanya kazi kubwa ya kujenga Zahanati kwa nguvu zao kwa kusaidiana na wafadhili marafiki kutoka Canada.
"Nimepokea kimemo wanasema wanahitaji jengo lingine liongezwe pale nikuhakikishie... Mita (Mgombea udiwani wa Kata ya Kahama, Samwel Mita) Ukifika huko anza kulidai hilo ili Zahanati hiyo iweze kupata hiyo huduma lijengwe jengo la akina mama kupumzikia pindi wanapoenda kliniki na kipaumbele kiwe ni kuweka jengo la mama na mtoto ili waweze kupata huduma hiyo bila shida, lakini nyie pia ni mashahidi kama mnakumbuka wakati tunaingia madarakani hakukuwa na hospitali ya wilaya lakini sasa hivi tunayo ," alieleza Dk.Mabula
Aidha aliongeza kuwa akipatiwa ridhaa atajikita kufanya mambo mbalimbali yakiwemo kutatua migogoro ya ardhi katika sekta ya ardhi, upimaji wa viwanja, sekta ya barabara, umeme, maji, elimu, mikopo sambamba na miradi ya kimkakati pia aliwaomba wavuvi kutumia fursa hiyo ili kukuza uchumi wao na wa Nchi.
Naye Mgombea udiwani wa Kata ya Kahama, Samwel Mita anaeleza kuwa ujenzi wa jengo la mama na mtoto atalipa kipaumbele ili kuondoa msongamano uliopo , kufatilia ili barabara inayoelekea hospitalini hapo ambayo imegeuka kuwa korifi inatengenezwa.
"Nikiingia madarakani wananchi wangu watarajie mambo makubwa sana sitowaangusha nitahakikisha miradi inayokuja kahama nitaisimamia kikamilifu" alieleza Mita.