Dk. Mahenge ataka walimu wawezeshwe

12May 2018
Ibrahim Joseph
DODOMA
Nipashe
Dk. Mahenge ataka walimu wawezeshwe

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Dk. Benilith Mahenge amesema silaha kubwa ya kupambana na kuondoa umaskini ni kuwawezesha walimu katika kazi yao.

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT), Mkoa wa Dodoma, Samweli Mkotya (wa pili kushoto), akisoma taarifa ya chama hicho mbele ya Mkuu wa Mkoa, Dk. Binilith Mahenge (kulia aliyekaa), walipofika ofisini kwake jana. PICHA: IBRAHIM JOSEPH

Dk. Mahenge aliyasema hayo wakati alipokutana na uongozi wa Chama Cha Walimu (CWT), jijini Dodoma jana Ofisini kwake waliofika kumpongeza kutokana kusaidia kutetea maslahi ya walimu.

Alisema ili taifa lolote liweze kuendelea silaha kubwa ya mapambano ya kuondoa umaskini ni kuwawezesha walimu katika kazi zao.

“Walimu ni watu mhimu wanatakiwa kujua bila wao Taifa haliwezi kuwa na wasomi bora maana wote wanapitia mikononi mwao hivyo wanatakiwa kuthaminiwa”alisema Dk. Mahenge.

Aidha,  aliwaomba walimu wote kuwa na ushirikiano katika maeneo yao ya kazi kwa kuwa ni  kioo katika jamaii kutokana na kuwategemea kwenye  kuwaelimisha.

Alisema serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli imeweka kipaumbele cha elimu na viwanda hivyo wasaidizi wake  na wananchi wengine  wanatakiwa kumuunga mkono katika kutatua changamoto hiyo.

Naye Mwenyekiti wa  CWT jiji la Dodoma,  Samwel Mkotya alisema chama hicho kinaongozwa na dira ya mpango mkakakati wa miaka mitano ambayo ni uwajibikaji, utawala bora, kupiga vita rushwa na matumizi mabaya ya madaraka na mali za chama.

Alimshukuru Mkuu huyo wa mkoa kwa kuvunja mkutano mkuu wa baraza la  CWT  taifa lililokuwa lifanyike mapema mwaka huu  kutokana na kujiridhisha kuwa kulikuwa na viashiria vya rushwa jambo ambalo lingesababisha kuwapata viongozi wasio na maadili na wapenda rushwa.

Mkotya alisema kitendo hicho kiliwakumbusha wanachama na viongozi wa CWT kukumbuka na kuheshimu misingi waliojiwekea katika utendaji wa kazi kama zilivyoanishwa  kwenye katiba yao ya kuhakikisha wanaelimisha jamii ili kuwatayarisha viongozi wazuri wa kesho.

Alimpongeza pia katika msimamo wake alioutoa siku ya wafanyakazi mwaka huu Mei Mosi alipokataa kupokea ahadi za zawadi kwa wafanyakazi bora jambo ambalo limewasaidia walimu kupata stahiki zao kutokana na kipindi cha nyuma kuambulia ahadi.

Hata hivyo,  Mkotya alimuahidi mkuu huyo  walimu wataendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha Watanzania wanapata elimu bora.