Dk. Mengi ataka kipaumbele wazawa ujenzi wa uchumi

12Apr 2017
Daniel Mkate
Dodoma
Nipashe
Dk. Mengi ataka kipaumbele wazawa ujenzi wa uchumi

MWENYEKITI wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TSPF), Dk. Reginald Mengi, amesema uchumi wa nchi yoyote duniani hujengwa na wazawa hivyo serikali inapaswa kuwaamini badala ya kuwakumbatia wawekezaji wa kigeni.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philipo Mpango (kushoto), Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage na Mwenyekiti wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Dk Regnald Mengi (kulia) wakifuatilia majadiliano katika mkutano baina ya sekta binafsi na serikali.

Akizungumza mjini Dodoma jana katika mkutano wa majadiliano kati ya serikali na sekta binafsi nchini, Dk. Mengi alisema iwapo viongozi watawaamini wawekezaji wazawa, ana imani kuwa dhamira ya serikali katika kukuza uchumi wa kati, kuelekeza Tanzania ya viwanda, itafanikiwa.

“Tunaiomba serikali iweze kutuamini wazawa. Sekta binafsi inakua kwa kasi, lakini kinachotakiwa ni kuweka ushirikiano kati ya serikali na taasisi yetu,” alisema na kusisitiza kuwa:

“Nchi yoyote haiwezi kujengwa na wageni bali wazawa iwapo watapewa kipaumbele na serikali katika kujenga uchumi wa nchi.”

Dk. Mengi alisema malengo ya sekta binafsi na serikali ni yale yale yakiwamo kuondoa umaskini, kutoa ajira na kuwapa maisha bora wananchi wake, hivyo kuiomba serikali kutoa kipaumbele kwa sekta binafsi ili wazawa washiriki katika kujenga nchi yao badala ya kuwaachia wageni.

“Tunaomba viongozi wawe na imani na wawekezaji wazawa, maana tunaweza kujenga nchi yetu wenyewe. Sote tuko katika meli moja kwani Rais (John Magufuli) amejipanga kuhakikisha tunajenga nchi kwa umoja,” alisema.

 Naye makamu Mwenyekiti wa TSPF, Salum Shamte alisema sekta binafsi iko tayari kushirikiana na sekta ya umma ili kuiweka nchi katika kiwango cha maendeleo ya juu kuelekea nchi ya uchumi wa kati wenye muktadha wa maendeleo ya viwanda.

Akizungumza katika mkutano huo, ulioandaliwa na mawaziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage na Dk. Philip Mpango wa Fedha na Mipango, shamte alisema pamoja na changamoto nyingi, wako tayari kushirikiana na serikali.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TSPF, Godfrey Simbeye, na wadau mbalimbali wa sekta hiyo, mawaziri, manaibu na wabunge.

Alisema sekta binafsi inakabiliwa na changamoto nyingi, lakini ziko tisa za msingi zikiwamo za kutokuaminiana kwa sekta hiyo na ile ya umma, kutokana na kushindwa kulipwa madeni yao pale wanapofuatilia kudai na kusababisha wengi kufunga shughuli zao.

Aidha, alisema changamoto nyingine ni upungufu wa ushirikishwaji unaohusu serikali, kutojali mikataba mbalimbali na kuchukuliwa kama uonevu pamoja na kutokuwa na uhakika wa umeme mkubwa viwandani.

Shamte alisema changamoto nyingine ambayo inaikabili sekta binafsi ni ongezeko la kero toka taasisi mbalimbali za serikali zikiwamo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), mamlaka ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi (Osha) na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Zimamoto ambazo zimekuwa zikidai fedha na kuonekana kama kodi.

“Changamoto nyingine ni upatikanaji wa mitaji ya fedha kutoka katika benki za kibiashara nchini,” alisema.

Hata hivyo, alisema mkutano huo wa majadiliano na serikali, unaonyesha kuwa matunda yameanza kuonekana yakiwamo ya kupungua kwa rushwa, kurudisha nidhamu kazini na kutilia mkazo wa ulipaji kodi.

Mafanikio mengine ni kuunda tume ya kuboresha biashara chini ya waziri mwenye dhamana ya viwanda, kutimiza ahadi ya elimu bure hadi kidato cha nne, ujenzi wa miundombinu mbalimbali, kuimarisha ushirikiano na kupunguza matumizi yasiyo la lazima, kutenga ardhi kwa wawekezaji na kusambaza umeme vijijini kwa asilimia 68 kupitia mradi unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Naye Waziri Mwijage alisema mkutano huo una lengo la kuongeza fursa ya maridhiano kati ya serikali na wafanyabiashara kupitia Baraza la Taifa la Biashara (TNBC).

Kwa upande wake, Dk. Mpango alisema serikali imedhamiria kujenga Tanzania mpya yenye sifa nne ikiwamo amani, usalama na utulivu.

Dk. Mpango alisema sifa nyingine ni utendaji wenye tija serikalini, nchi yenye uchumi imara, mazingira bora ya kufanya biashara na wananchi wake wawe na maisha bora hasa wale wanaoishi vijijini.

Habari Kubwa