Dk. Mengi kinara wa wafuasi twitter

17Jun 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Dk. Mengi kinara wa wafuasi twitter

MWENYEKITI Mtendaji wa IPP Limited na mfanyabiashara maarufu nchini, Dk. Reginald Mengi, ametajwa kuwa mtu mwenye wafuasi wengi katika mtandao wa kijamii wa twitter, akiwa na zaidi ya watu milioni moja.

Hadi jana saa 7:30 mchana, Dk. Mengi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) alikuwa na wafuasi 1,020,530.

Kwa mujibu wa kampuni ya uchambuzi wa masuala ya kijamii ya socialbakers.com, akaunti ya twitter ya Dk. Mengi ni ya 13 katika zile zenye wafuasu wengi barani Afrika hivyo kumfanya kuwa mfanyabiashara kinara wa mtandao huo katika Afrika Mashariki.

Wafanyabiashara wengine mashuhuri Afrika ambao hutumia mtandao wa twitter ni pamoja na kinara wa matajiri barani na mmiliki wa kundi la kampuni za Dangote, Aliko Dangote, raia wa Nigeria. Wengine ni bilionea wa Zimbabwe anayemiliki kampuni ya simu ya Econet Wireless, Strive Masiyiwa, Tony Elumelu wa Nigeria, Vimal Shah na Chris Kirubi wote wa Kenya.

Tangu ajihusishe na mtandao wa Twitter Januari, 2012, taarifa nyingi anazozitoa katika ukarasa wake ni zile zinazowafundisha na kuwaasa vijana kujihusisha na biashara halali na kwa uadilifu.

Kwa mujibu wa taasisi hiyo, Dk. Mengi katika ukurasa wake huo, pia amekuwa akichangia masuala ya kisiasa na kijamii akilenga zaidi kupiga vite vitendo vya rushwa.

Nchini Tanzania, twitter imeonekana kuwa ndio makini katika uchambuzi na maoni juu ya masuala mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kiuchumi kulinganisha na mitandao mingine ya kijamii kama vile Facebook and instagram.

Katika uchambuzi mbalimbali uliopita juu ya matumizi ya twitter, ulionyesha kuwa unatumiwa zaidi katika nchi za Misri, Nigeria, Afrika Kusini, Kenya and Ghana.

Pia mtandao huo umekuwa maarufu na makini katika mawasiliano. Ofisa wa twitter, Sarah Harte, alipoulizwa kuhusu takwimu za Tanzania katika matumizi ya mtandao huo, alisema kwa kawaida imekuwa haitoi idadi halisi lakini akasema kwa duniani, twitter imekuwa ikitumiwa na zaidi ya watu milioni 328 kila mwezi huku zaidi ya watu milioni 500 wakiwa si hai mara kwa mara.

Habari Kubwa