Dk. Mpango kuhudhuria misa ya kumbukumbu ya Hayati Mkapa

21Jul 2021
Abdallah Khamis
Mtwara
Nipashe
Dk. Mpango kuhudhuria misa ya kumbukumbu ya Hayati Mkapa

MAKAMU wa Rais Dk. Philip Mpango, anatarajiwa kuwasili mkoani Mtwara Julai 23, 2021 kwa ajili ya kuwaongoza Watanzania kwenye misa ya kumbukumbu ya kutimiza mwaka mmoja tangu kufariki kwa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamini Mkapa.

Dk. Mpango pamoja na kuhudhuria misa hiyo, atazindua miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wakazi wa mkoa wa Mtwara, katika ziara ya siku tano.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mkuu wa mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali, Marco Gaguti, amesema Makamu wa Rais atakuwa wilayani Masasi kwenye kijiji cha Lupaso kwa ajili ya kuhudhuria misa hiyo.

“Siku hiyo hiyo baada ya misa makamu wa rais atazindua soko katika wilaya ya Masasi na siku inayofuata atazindua kiwanda cha kubangulia korosho katika wilaya ya Newala, kiwanda hiki kina thamani ya zaidi ya Shs. Mil 800/-,” amesema.

Ameongeza kuwa Julai 26 makamu wa rais ataweka jiwe la msingi katika hospitali ya rufaa kanda ya kusini na Julai 27 atamaliza ziara yake mkoani humo

Amesema makamu wa rais atasimama kusalimia wananchi katika wilaya ya Tandahimba na kuzungumza na wakazi wa wilaya ya Mtwara Mjini katika uwanja wa Sabasaba.

Gaguti, ameowaomba wananchi wajitokeza kwa wingi kumpokea makamu wa rais, huku wakiwa wamechukua tahadhari zote za kujikinga na maaambukizi ya maradhi ya corona.