Dk. Mwinyi awatwisha zigo mawaziri

23Nov 2020
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe Jumapili
Dk. Mwinyi awatwisha zigo mawaziri

NI mzigo mzito. Ndivyo inavyoweza kuelezwa baada ya rais wa Zanzibar, Dk. Hussien Mwinyi, kuwapa maagizo 13 mawaziri aliowateua na kuwaapisha jana huku akionyesha hana mzaha na atakayekwenda kinyume cha hayo.

Katika hafla ya kuwaapisha iliyofanyika Ikulu, Zanzibar, Dk Mwinyi aliwataka mawaziri 13 kutekeleza maagizo 13 ambayo kwa kiasi kikubwa yanaonekana ni mzigo mkubwa kwao maana amesema atakayeshindwa kutekeleza atamwondoa.

Alisema mkataba wake na watendaji aliowateua, wakiwemo mawaziri, ni kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kikamilifu na hatasita kumwondoa yeyote atakayeshindwa kuwajibika.

Dk. Mwinyi aliwaagiza mawaziri hao kila mmoja kuhakikisha anaijua wizara yake na taasisi zilizomo katika wizara husika haraka iwezekanavyo na kuanza kazi mara moja, kutengeneza mpango kazi wenye bajeti kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hotuba yake ya ufunguzi wa Baraza la Wawakilishi na ahadi zake alizozitoa wakati wa kampeni.

Pia aliwataka kuwashirikisha wadau katika taasisi mbalimbali ili kupata maoni yao kwa sababu huwezi kutekeleza kazi kwa ufanisi bila ya kuwashirikisha wadau.
 
“Natoa mfano kama Wizara ya Elimu ina wadau wengi ambao wanaweza kutoa maoni mazuri. Washirikishe, chukua maoni ya wadau, huwezi kufanya kazi vizuri kama hujakutana na chama cha walimu. Mhakikishe kila mmoja anakutana na wadau,” alisema.
 
Alisema dira ya maendeleo iwe kigezo cha mpango kazi wao wenye bajeti kwa sababu mpango bila ya bajeti ni rasimu isiyofaa.

MIRADI YA WIZARA

Pia aliwataka kutembelea miradi yote iliyomo katika wizara zao na kujiridhisha na kiwango cha ubora wake, utaratibu wa zabuni uliotumika, malipo kwa makandarasi, na muda wa kukamilisha mradi husika.
 
”Katika hili nataka nitolee mifano kwa siku chache nilizokaa ofisini. Nilitembelea baadhi ya maeneo nimesikitishwa sana na kiwango cha miradi tunayoifanya. Mathalani nimekwenda katika Hospitali ya Mnazi Mmoja tuna mradi pale wa jengo la macho, kuna jengo la kisasa la kufanya upasuaji wa macho mpaka leo halifanyi kazi sababu kuna beseni moja la madaktari kujiosha kabla ya kuingia katika upasuaji halijawekwa. Haiwezekani haya ndiyo tunayoyasema hatuwezi kukubali mambo ya namna hii.
 
“Nimekwenda bandarini nikaambiwa moja ya sababu ya mizigo kuchelewa kutoka ni kwamba kuna baadhi ya wafanyabiashara wanachelewa kuchukua mizigo yao, wanaifanya bandari kuwa sehemu ya kuhifadhia bidhaa zao. Nikauliza ni hatua gani mlizozichukua nikaambiwa kuwa Saateni lipo ghala la kuhifadhia mizigo nikasema twendeni lakini jengo hilo limechelewa kukamilika na mkandarasi ameshalipwa fedha zote. Iwe ni mwisho katika mambo haya,” alisema.
 
Pia alisema juzi Makamu wa Pili wa Rais alifanya ziara katika mradi wa uzalishaji wa vifaranga vya samaki lakini hakuna uzalishaji unaofanywa, hivyo akataka apewe ripoti ya kina kuhusu mradi huo.
 
UWAJIBIKAJI

Aliwataka mawaziri hao kuwa watendaji na kila mfanyakazi kuhakikisha anawajibika kwa kazi aliyopewa ili huduma zinazotolewa kwa wananchi ziwe bora na kisasa na kusiwe na malalamiko.
 
Dk. Mwinyi alisema kuna maeneo mengi bado huduma ni duni, watu hawawajibiki na huduma zinazotakiwa kutolewa hazitolewi, hivyo akawataka mawaziri kwenda kufanya kazi na kuhakikisha haki za watu zinatolewa.
 
“Mfano kuna malalamiko makubwa katika Wizara ya Ardhi, watu wananyang’anywa ardhi zao, hakikisheni mnaondoa matatizo kwa kuweka mfumo mzuri wa kukutana na wananchi kuwasikiliza shida zao. Ninataka taarifa karibu na uchaguzi kuna ardhi nyingi zimetolewa nataka orodha ya yote hayo,’ alisema.

RUSHWA NA UBADHIRIFU

Alieleza kuwa kuondoa rushwa na ubadhilifu kwa sababu kuna rushwa na ubadhilifu mkubwa unaofanywa katika upotevu wa mali za serikali.
 
Alisema kuna baadhi ya wizara kuna makusanyo lakini fedha hazikusanywi, kuna fedha za bajeti zinazoibiwa, kuna fedha zinazopelekwa katika miradi lakini miradi hiyo haitekelezwi hivyo kuondoa wizi katika wizara zao.
 
“Waziri ukishindwa kushughulikia hayo maana yake hunifai na bahati nzuri. Mkataba tuliotia saini leo (jana) hauna muda. Ukifanya vizuri utabaki na ukifanya vibaya utaondoka. Naomba tusifichane, niliwaahidi wananchi sitakuwa na huruma na muhali hivyo nitaanza na ninyi mawaziri”alisema.
 
MAKUSANYO YA MAPATO

Alisema ukusanyaji wa fedha za mapato wizara zenye kukusanya mapato ikiwamo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), haufanyiki ipasavyo na kumtaka Waziri wa Fedha kuvifuatilia vyombo hivyo. Alisema fedha nyingi zinapotea na kumtaka kurekebisha hali hiyo mara moja.
 
UBUNIFU, KUACHA URASIMU

Dk. Mwinyi aliwataka kuwa wabunifu kwa kubuni mbinu mpya zitakazoleta ufanisi hivyo kuwatumia wataalamu katika wizara zao kubuni njia mpya za kufanya kazi.
 
Alisema kuna urasimu mkubwa, hivyo hauna budi kuondolewa katika kupata huduma kwa sababu wananchi wanazungushwa katika kupata huduma mbalimbali.
 
“Nataka mwondokane na tatizo la urasimu katika kutoa huduma wa lile tatizo la njoo kesho liwe basi tena. Watendaji muwe tayari kujibu barua na maombi ya wananchi na sio kukaa kimya,''alisema.

“Mambo yenye maslahi ya umma yasicheleweshwe, muda wetu ni miaka mitano hatuna muda mwingine. Msikae mkasema mtafanya mwakani anzeni kufanya sasa. Toeni uamuzi kwa mambo yenye maslahi ya umma,” alisema.
 
Sambamba na hilo, aliwataka kuwa wepesi wa kupeleka mapendekezo kubadilisha sheria kama sheria husika ni kikwazo kwa sababu kuna baadhi ya matatizo yanasababishwa na sheria zilizopo na kutolea mfano wa masuala ya udhalilishaji, hivyo kuangalia sheria zinazokidhi kukomesha vitendo hivyo.
 
UTOAJI TAARIFA

Aliwataka kutoa taarifa za kazi wanazozifanya kwa waandishi wa habari hivyo kuhakikisha wanakua marafiki na waandishi wa habari hakuna haja ya kuficha wanachokifanya na kuelezea mafanikio na changamoto na si kuwakimbia waandishi.
 
Aliwataka kusikiliza malalamiko ya wananchi na kila wizara kuwa na utaratibu wa kusikiliza malalamiko ya wananchi na kuyatafutia ufumbuzi.

AAHIDI USIKIVU

Dk Mwinyi aliwataka mawaziri hao kuanza kazi na yuko tayari kusikiliza kikwazo chochote, hivyo kumweleza na kuchukua hatua kwa yale ambayo yapo nje ya uwezo wao katika kuchukua hatua.
 
Alisema amekamilisha safu ya mawaziri na kwamba matarajia ya wananchi kwao ni makubwa, hivyo wale mawaziri wazoefu waendelee kuonyesha uzoefu wao na wale wapya wakahakikishe wanaleta utendaji mpya.
 
“Waheshimiwa Mawaziri nakupeni hongera sana lakini wakati huo huo  nawapeni pole kwa sababu mzigo niliokupeni ni mkubwa, hivyo hakikisheni mnatekeleza wajibu wenu,’ alisema.
 

Habari Kubwa