Dk. Shein ajivunia ongezeko mapato

13Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Zanzibar
Nipashe Jumapili
Dk. Shein ajivunia ongezeko mapato

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema ongezeko la makusanyo ya mapato limesababisha kuimarika kwa uchumi.
Dk. Shein aliyasema hayo jana katika uwanja wa Gombani, Mkoa wa Kusini Pemba katika Kilele cha Sherehe za Miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, picha mtandao

Alisema katika mwaka 2017/18, Sh. bilioni 688.7 zilikusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) ikilinganishwa na Sh. bilioni 521.8 zilizokusanywa na taasisi hizo kwa mwaka wa fedha wa 2016/17.

Kwa mujibu wa Dk. Shein, kiwango hicho ni ongezeko la Sh. bilioni 166.9 sawa na asilimia 32 na mafanikio hayo yameiwezesha serikali kutekeleza mipango yake ya kuinua uchumi na kuwasogezea wananchi huduma za kijamii kwa wepesi na kwa ufanisi mkubwa.

Dk. Shein alisema uchumi ulikua kwa asilimia 7.7 mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 5.8 mwaka 2016 wakati pato la mtu binafisi liliongezeka hadi Sh. milioni 2.1 kwa mwaka 2017 ikilinganishwa na Sh. milioni 1.89 mwaka 2016.

Aidha, Dk. Shein alisema mfumuko wa bei nao uliendelea kudhibitiwa katika tarakimu moja katika mwaka 2018 hadi asilimia 3.9 ikilinganishwa na asilimia 5.6 katika mwaka 2017.

“Mafanikio hayo yamechangiwa na juhudi mbalimbali za serikali ikiwemo wazalishaji wa ndani na kuweka mazingira mazuri ya biashara katika uagizaji na usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi,” alisema.

Dk. Sheina alisema katika kipindi cha miaka 55 ya Mapinduzi, kumekuwa na mafanikio makubwa ikiwamo kuimarika kwa huduma za elimu kwa kuwa kabla ya Mapindzi ya 1964 huduma hizo zilikuwa chache na zilitolewa kwa ubaguzi na wachache waliopata fursa ya elimu walilipia.

Alisema kwa sasa serikali inaendelea na uamuzi wake wa kuwapa wananchi matibabu bure lengo likiwa kuhakikisha kuwa wananchi wote wa Unguja na Pemba wanapata huduma za kinga na tiba kwa ajili ya kuendeleza afya na kusisitiza kuwa serikali itafanya kila iwezalo ili huduma za afya ziendelee kuwa bure.

Kuhusu mafanikio, alisema serikali imeongeza kasi ya kusambaza umeme mijini na vijijini na kwamba hadi Desemba, mwaka jana vijiji 2,694 kati ya 3,259 vya Unguja na Pemba, sawa na asilimia 83 vimepatiwa umeme.

Pia alisema sekta ya utalii imeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka, huku idadi ya watalii ikiongezeka. Alisema mwaka jana watalii 520,809 waliwasili nchini, ikilinganishwa na 433,116 mwaka 2017, ikiwa ni ongezeko asilimia 20.

Alisema lengo la serikali la kufikia watalii 500,000 kwa mwaka ifikapo mwaka 2020 lengo hilo litafikiwa.

Mapema Dk. Shein alipokea maandamano ya wananchi kutoka wilaya zote za Unguja na Pemba, yakifuatiwa na wafanyakazi kutoka taasisi, idara na wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, waliovalia sare za miaka 55 ya Mapinduzi hayo.

Sherehe hizo zilinogeshwa na gwaride rasmi lililoandaliwa na kushirikisha vikosi vya ulinzi na usalama vikiwamo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Mafunzo, KMKM, Zimamoto na KZV, ambavyo vilipita mbele ya mgeni rasmi na kutoa heshima kwa mwendo wa pole na haraka.

Habari Kubwa