Dk.Nchemba: Mikopo sekta binafsi yaongezeka

10Jun 2021
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Dk.Nchemba: Mikopo sekta binafsi yaongezeka

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa wastani wa asilimia 4.8 katika kipindi cha mwaka unaoishia Aprili 2021 ikilinganishwa na ukuaji wa wastani wa asilimia 5.8 katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2020.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba.

Amebainisha kuwa sehemu kubwa ya mikopo ilielekezwa katika shughuli  binafsi ambazo zilipata asilimia 35.8 ya mikopo yote ikifuatiwa na shughuli za biashara asilimia 15.7, uzalishaji viwandani asilimia 10.1 na kilimo asilimia 8.

Dk. Nchemba ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akiwasilisha bungeni hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2020 na mpango wa maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2021/22.

“Kwa upande wa ukuzaji rasilimali mwaka 2020,  ukuzaji rasilimali kwa bei za miaka husika ulifikia Shilingi 59.2 trilioni  kutoka Shilingi 55.8 trilioni za mwaka 2019 ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 6.2, huku ukuzaji wa rasilimali za kudumu kwa bei za miaka husika uliongezeka kwa asilimia 7.8 kutoka Sh59.4 trilioni mwaka 2019 hadi Shh64.0 trilioni mwaka 2020.” amesema.

Habari Kubwa