Dodoma hali sio nzuri chukueni tahadhari –RC Mtaka

03Aug 2021
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Dodoma hali sio nzuri chukueni tahadhari –RC Mtaka

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka, amewataka wakazi wa Mkoa huo kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona kwa sababu hali iliyopo katika Mkoa huo si nzuri.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka.

Mtaka amesema hayo leo Agosti 3, 2021 wakati akizungumza na Askari wa Usalama wa Barabarani na viongozi wa masoko mkoani humo.

Aidha, amewataka askari, viongozi wa masoko na wafanyabiashara kuhakikisha wanachukua hatua za kujikinga katika maeneo yao kwa kuvaa barakoa na kunawa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono.

Pia amewataka askari wa usalama wa barabarani kuhakikisha watu wote wanakaa kwenye viti (level seat) kwenye daladala na bajaji na kwenye bodaboda kuhakikisha hawabebi abiria zaidi ya mmoja.

Kwa Upande wake, Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma, Boniface Mbao, amesema watakapotoka katika kikao hicho wataenda kutekeleza maagizo hayo kwa kutoa elimu na ikibidi kwa ukali, ili kuhakikisha abiria wanakaa katika viti kwenye mabasi ya abiria.

Mbao amesema hakuna gari litakalopita kwenye Mkoa huo likiwa limejaza zaidi ya abiria waliokaa kwenye viti.