Dozi chanjo ya corona mbioni kumalizika Dar

10Oct 2021
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Dozi chanjo ya corona mbioni kumalizika Dar

MGANGA Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Rashid Mfaume, amesema chanjo 160,000 walizopewa aina ya Johnson & Johnson ziko mbioni kumalizika baada ya kuongezeka kwa mwamko wa uhitaji wa huduma hiyo.

Aliyataja mambo yaliyochangia wakazi wa mkoa huo kuchangamkia chanjo hizo kuwa ni huduma ya mkoba ya nyumba kwa nyumba, kuongezeka kwa vituo vya kutolea chanjo kutoka 28 hadi 318 na elimu inayoendelea kutolewa na vyombo vya habari.

Dk. Mfaume aliyaeleza hayo jana mkoani Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Tiba Shufaa Duniani yenye kaulimbiu inayosema 'usimuache yeyote nyuma, usawa katika utoaji wa huduma za tiba shufaa.

Alisema uhitaji wa chanjo kwa wakazi wa mkoa huo ni mkubwa, hali ambayo inatia moyo kwa wataalamu wa afya kuona kuna mwamko mkubwa tofauti na siku za awali.

"Kati ya chanjo 160,000 tulizopewa mkoa wetu, zilizobaki ni kidogo sana na wiki hii tunatarajia kuzimalizia na tutaendelea kutoa huduma kwa sababu kuna chanjo nyingine serikali imezipokea jana (juzi) kutoka kwa marafiki zetu, Serikali ya China," alisema Dk. Mfaume.

Akizungumzia Tiba Shufaa, alisema ni asilimia 14 ya wagonjwa waliofikiwa na huduma hiyo kati ya wagonjwa wengi wanaostahili kuipata, kunakosababishwa na uhaba wa watoa huduma.

Aliwataka viongozi wa dini waendelee kushirikishwa kikamilifu katika kutoa Tiba Shufaa kwa sababu wana mchango mkubwa katika kuponya kwa njia ya imani.

Alisema pia kuongeza uelewa kwa kundi la watoa huduma na kupeleka taarifa kwa jamii kuhusu matumizi Tiba Shufaa ili jamii iwe na uelewa mpana katika kusaidia upatikanaji wa huduma hiyo.

Dk. Mfaume alisema Mkoa wa Dar es Salaam watatoa elimu kuhusu Tiba Shufaa kwa lugha rahisi na kuwafikia wananchi wengi katika kurahisisha upatikanaji wake.

Meneja Mpango wa Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Omary Ubuguyu, alisema wamekutana kwa ajili ya kupitia mwongozo na sera za Tiba Shufaa kwa sababu wameona kuna uhitaji mkubwa wa kuupitia na kufanya maboresho.

Alisema wanatakiwa kujenga hamasa kuhusu huduma za Tiba Shufaa zinazotolewa nchini na wanajamii, wataalamu wa afya na viongozi wa dini ili itolewe sambamba na tiba nyingine.

Alisema kundi kubwa la wagonjwa wanaotakiwa kupatiwa Tiba Shufaa halijafikiwa kwa sababu kati ya watu milioni tisa wanaougua magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ni watu milioni tatu hadi tano wanaopata huduma hiyo.