DP, NRA, AAFP vyafungua pazia uchukuaji fomu urais

06Aug 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
DP, NRA, AAFP vyafungua pazia uchukuaji fomu urais

PAZIA la uchukuaji fomu kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lilifunguliwa jana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), huku wagombea watatu kutoka vyama mbalimbali vya siasa wakichukua fomu na kutamba kuingia Ikulu.

Kwa mujibu wa tume hiyo uchukuaji fomu ulianza jana hadi 25, mwaka huu katika Ofisi za NEC zilizopo jijini hapa.

Wagombea hao walianza kuwasili katika Ofisi za NEC kuanzia saa 4:30 asubuhi, ambapo mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia AAFP, Seif Maalim Seif alikuwa wa kwanza kufika akiwa ameambatana na Mgombea Mwenza wake, Rashid Ligania Rai na wanachama.

Mgombea wa pili wa DP, Philipo Fumbo aliwasili saa 5:30 asubuhi bila mgombea mwenza, Zainab Juma Hamisi na wapambe wake wanne.

Mgombea wa tatu wa NRA, Leopord Mahona aliwasili saa 6:30 mchana akiwa na wapambe wawili bila mgombea mwenza, Hamis Ali Hassan.

Wagombea hao walikabidhiwa fomu hizo na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage.

KAULI YA MGOMBEA AAFP

Akizungumza nje baada ya kukabidhiwa fomu, mgombea huyo aliwaahidi Watanzania kuwa ataleta mabadiliko ya kweli.

“Nakwenda kutafuta wadhamini na kurejesha fomu, hatua itakayofuata ni kuingia Ikulu, tuna imani na Tume katika kusimamia suala zima la uchaguzi, tunahitaji mabadiliko ya kweli yanayoathiri mwananchi mmoja mmoja kwa kila siku, AAFP tunaamini tuna uwezo, sababu na utayari wa kuleta hali bora zaidi kuliko ilivyosasa iwe kiuchumi, kijamii na muktadha mzima wa kimaendeleo,” alisema.

MGOMBEA DP ANENA

Mgombea Fumbo, alisema chama hicho ndio kinachosikilizwa kwa kuwa ni cha walala hoi, hivyo watafanya maajabu ya ‘Njiti ya kiberiti kuwasha msitu’.

“Tunatakiwa tukatafute wadhamini, na kwenda mikoani sina shaka kwa kuwa nina wadhamini wa kutosha nitamaliza zoezi hili haraka maana chama hichi kina mila tofauti na vyama vingine vya siasa, hivyo baada ya kupata wadhamini na kurudisha fomu, DP itawasha moto maana baada ya kuteuliwa ni saa ya ukombozi,” alisema.

MGOMBEA NRA AFUNGUKA

Mgombea NRA, Mahona alisema huo ni mwanzo wa utumishi wake kwa nchi na ni safari nzuri na ya matumaini kwa Watanzania ambayo itawahakikishia kuwa yaliyopita sasa yamepita.

Alitoa wito kuwe na uchaguzi huru ili Watanzania wapate kiongozi wanayemtaka.

UFAFANUZI WA NEC

Akitoa maelezo ya awali kabla ya kukabidhiwa fomu hizo, Mkurugenzi wa Tume hiyo, Dk. Wilson Charles Mahera, alisema watatakiwa kudhaminiwa na wapigakura wasiopungua 200 ambao wamejiandikisha kupiga kura katika kila mkoa kwenye mikoa 10 na kati ya hiyo angalau miwili kutoka Zanzibar.

Ratiba uchukuaji fomu

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Tume hiyo, leo wagombea wa UPDP na Demokrasia Makini watachukua fomu.

Pia, Agosti 7, mgombea wa Chama cha ADC atachukua fomu huku wa CHADEMA atachukua Agosti 8, mwaka huu.

Agosti 11, wagombea wa UMD na CUF na Agosti 12 ni zamu ya CCK.

Habari Kubwa