DPP akosolewa kukusanya fedha za uhujumu uchumi

12May 2021
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
DPP akosolewa kukusanya fedha za uhujumu uchumi

​​​​​​​WAKILI wa kujitegemea, Peter Madeleka, amesema Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hapaswi kukusanya fedha za makosa ya uhujumu uchumi kwa mujibu wa kanuni ya 21, kanuni ndogo 3 (a) ya Kanuni ya Sheria za Kukiri Makosa (Pre Beginning) ya mwaka 2021.

Peter Madeleka.

Amesema kanuni hiyo imeeleza wazi kuwa, anayepaswa kukusanya fedha hizo ni Msajili wa Hazina na kwamba kwa kufanya hivyo anakiuka sheria.

Aliyaeleza hayo jana Dar es Salaam, katika mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu makosa yanayofanywa kwenye Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi nchini, akiwa mmoja wa watuhumiwa waliokaa gerezani zaidi ya mwaka mmoja akakiri kosa, akalipa fidia na kuachiwa.

"DPP hajui kama hapaswi kupokea fedha kwa niaba ya hazina," alsema Wakili Madeleka.

Alisema Kanuni ya Sheria ya Kukiri Makosa (Pre Beginning) siyo inamtaka mtuhumiwa kulipa fedha kwa DPP bali inamtaka mtuhumiwa kufanya naye maridhiano ya kuomba kupunguziwa adhabu endapo atawataja watuhumiwa wenzake ili nao wakamatwe walipe fidia.

"DPP anaifanya 'Pre beginning' kama ni makubaliano ya kukusanya fedha wakati DPP siyo TRA (Mamlaka ya Mapato nchini)," alifafanua.

Kuhusu Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi, alisema haina upungufu isipokuwa watendaji wanaoisimamia hawana uelewa wa kutosha katika kiisimamia na kuitekeleza.

"Ukiniuliza Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi mimi natakuambia ipo sawa kabisa tatizo lipo kwa vyombo vinavyoisimamia havina uelewa wa kutosha," alisema Wakili Madeleka.

Alisema Jeshi la Polisi ambao ndio wanaotakiwa kufanya upelelezi wa kesi hawana uelewa wa sheria hiyo ndio sababu wahusika wanasota magereza wakisubiria kukamilika.

Alishauri kuwa wanazosimamia sheria wanapaswa kuzisoma na kuzielewa kwanza kabla ya kuzitekeleza.

Habari Kubwa