DPP aanika vikwazo 3 kesi za ufisadi

06Feb 2016
Salome Kitomari
Nipashe
DPP aanika vikwazo 3 kesi za ufisadi

MWENDESHA Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP), Biswalo Mganga amesema kukosekana kwa uzalendo, athari za rushwa na woga ni miongoni mwa vikwazo vitatu vinavyokwamisha ushahidi.

Na mwishowe kuchelewesha majalada ya mashtaka ya kesi mbalimbali, zikiwamo kubwa za ufisadi unaoligharimu taifa mabilioni ya fedha.

Akizungumza na Nipashe mwishoni kwa wiki jijini Dar es Salaam, DPP Mganga alisema anaendelea kufanya kazi kwa weledi ili kuhakikisha kuwa wanakabili changamoto hizo na mwishowe wanatimiza malengo waliyojiwekea. Kwa muda mrefu, baadhi ya wanasiasa na wanaharakati mbalimbali akiwamo aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha DP, Marehemu Mchungaji Christopher Mtikila, wamekuwa wakiitupia lawama ofisi ya DPP kuwa inachangia kushamiri vitendo vya rushwa na ufisadi nchini kwa kukaa muda mrefu na mafaili bila ya kufikisha mahakamani watuhumiwa wa kashfa mbalimbali. Hata hivyo, DPP Biswalo alisema kukosekana ushahidi wa kutosha kunakosababishwa na vikwazo vitatu, ndiyo chanzo cha kuchelewa kwa majalada ya kesi mbalimbali kufikishwa mahakamani kwa ajili ya kuwatia hatiani wahusika wa vitendo vya rushwa na ufisadi. Alisema kwa kawaida, kama hakuna ushahidi wa kutosha, serikali huishia kushindwa mahakamani na hivyo kuiongezea mzigo kwani kila kesi huwa na gharama zake. DPP Mganga alikitaja kikwazo kikubwa kuwa ni hulka ya Watanzania walio wengi kutotaka kutoa ushahidi katika kesi mbalimbali, zikiwamo zile zenye maslahi mapana kwa taifa. Akieleza zaidi kuhusiana na kikwao hicho, Mganga alisema wakati mwingine huwapata watu wanaotoa ushirikiano wa kutosha wakati wa hatua za upelelezi, lakini inapokuja hatua ya kutakiwa kutoa ushahidi huo mahakamani, baadhi ya watu hao hukataa kufanya hivyo kwa sababu mbalimbali ikiwamo ya woga au rushwa na hivyo kukwamisha maendeleo ya jalada la kesi husika. "Ni vigumu kwa DPP kumpeleka mtu mahakamani bila kujiridhisha na kilichopo kwenye makaratasi na mashahidi waliopo," alisema Mganga. "Ikumbukwe kuwa wakati kosa linatendeka DPP huwa hayupo… anasoma tu kwenye makaratasi na kusikiliza mashahidi ili kupata ukweli. "Tunafanya hivyo ili kuhakikisha kuwa anayefikishwa mbele ya vyombo vya sheria ni yule aliyetenda kosa na kwamba, hata unapokaa nafsi haikusuti kuwa (kuna mtu) ulimuonea." Msingi wa kesi mara zote ni ushahidi wa vielelezo, alisema, na mashahidi wa kuzungumza mbele ya mahakama. “Inapotokea Watanzania wameona kosa likitendaka lakini hawataki kwenda kutoa ushahidi, hicho ni kizingiti kikubwa kwa DPP kutekeleza wajibu wake.” KIKWAZO CHA PILI Kwa mujibu wa DPP, kikwazo cha pili kinachokwamisha kufikishwa mahakamani kwa majalada ya kesi kubwa ni uwajibikaji usiofikia viwango wa watumishi wenye dhamana ya kusimamia maeneo mbalimbali ya taasisi za umma au chombo fulani na kwamba, ni lazima kila mmoja awajibike kwa maslahi ya Watanzania na kuacha ubinafsi ili kuondokana na kikwazo hiki. Akifafanua kuhusu kikwazo hicho, DPP alitaja mfano wa athari zitokanazo na uzembe au kutowajibika ipasavyo kwa sababu yoyote ile kunakofanywa na mpelelezi wa kesi fulani. Alisema kama mpelelezi anaamua kutofanya kazi yake ipasavyo au kuharibu upelelezi na kupeleka ushahidi mwepesi kwa DPP ili utumike kuandaa mashtaka dhidi ya mtuhumiwa fulani, ni wazi kwamba katika kesi ya namna hiyo, serikali itashindwa kutokana na ushahidi dhaifu na wahalifu kuachwa huru. "Huyu mpelelezi wa aina hii (anayeandaa ushahidi dhaifu) ni Mtanzania. Anapaswa kutimiza wajibu wake ipasavyo kuisaidia ofisi ya DPP, lakini kwa maslahi binafsi, anaharibu (ushahidi) na kutoa mwanya kwa mtuhumiwa kuendelea kuwapo uraiani bila kuchukuliwa hatua yoyote," alisema Mganga. "Hiki pia ni kikwazo kikubwa." DPP Mganga alitoa mfano mwingine wa kikwazo cha pili kuwa ni katika ngazi ya Mahakama, akisema kama hakimu au jaji atatoa uamuzi wa kesi kwa maslahi binafsi kwa kuwa amepewa rushwa ili apindishe sheria, ni wazi kuwa DPP atakwama katika kesi husika na mwishowe serikali kuonekana imeshindwa. "DPP hawezi kufanikiwa (katika kazi yake) bila kuwa na wapelelezi wazuri na mahakimu na majaji wanaotekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria pasipo kushawishiwa na chochote," alisema. KIKWAZO CHA TATU DPP alizunguzmia hulka ya kinafiki kwa baadhi ya Watanzania na kupenda kulaumu kuliko kulisaidia taifa katika harakati za kukomesha maovu. "Unabaki kulaumu na kutanguliza ubinafsi badala ya kusaidia utatuzi. Lazima tubadilike kifikra. Tuipende Tanzania na kurudi kwenye Utanzania wetu, tuache kujifikiria wenyewe bali na wengine katika kunufaika na raslimali za taifa," alisema. Alisema daima, ofisi yake inatimiza wajibu wake kuhakikisha hakuna mtu wa kujinufaisha na uhalifu na kila mtu ataadhibiwa kwa kile alichokitenda, iwe ni rushwa, ufisadi, wizi na maovu mengine ambayo siyo ya manufaa kwa Watanzania. Mkurugenzi huyo wa mashtaka alisema wanaotenda makosa ni Watanzania wanaoishi katika jamii, lakini kinachoonekana ni kukosekana kwa uzalendo kwani yapo makosa yanatendwa nchini na raia wa kigeni kwa kushirikiana na wenyeji kama inavyotokea katika utoroshaji wa nyara za serikali kama wanyamapori. AFAFANUA ZAIDI KUHUSU KESI Kuhusiana na kesi mbalimbali kupelekwa mahakamani, alisema ofisi yake inajitahidi na kila inapojiridhisha na ushahidi, jalada husika hupelekwa mahakamani na yale ambayo yanahitaji kurudi kwenye vyombo vya uchunguzi zaidi, inafanyika hivyo ili kuwa na ushahidi wa kuwatia hatiania wahusika. Alisema sheria inatoa siku 60 kwa DPP kulifikisha mahakamani jalada la kesi linapopelekwa kwake, lakini inategemea amepokea majalada mangapi kwani wakati mwingine yanaweza kuwa 30 ambayo yakigawanywa kwa wastani wa siku 60, maana yake kila moja lishughulikiwe kwa siku mbili, huku mengine yakitakiwa kurudishwa kwenye vyombo vya uchunguzi kwa upelelezi zaidi. "Wakati mwingine tunaweza kulaumiwa lakini tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria. Unaletewa majalada 30 na una siku 60 za kuyasoma na kuandaa mashtaka na pia kujiridhisha na ushahidi ili kesi iende mahakamani. Ni lazima kuwe na muda zaidi kulingana na kesi husika, nyingine ni nzito sana na zinahitaji umakini wa hali ya juu," alisema. DPP Mganga alisema wameimarisha ushirikiano wa karibu baina ya ofisi yake na wakuu wa vyombo vya uchunguzi wakiwamo Mkurugenzi wa Upelelezi (DCI) na Mkurugeniz wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa kila mmoja anatimiza wajibu wake ipasavyo na mwishowe kufanikisha malengo. Hivi karibuni, DPP alikutana na DCI na Mkurugenzi wa Takukuru na kufanya mkutano wa pamoja na waandishi wa habari kueleza mikakati ya kushirikiana katika kuharakisha upelelezi na uandaaji wa mashtaka kwa ajili ya kuwafikisha wahusika mahakamani. Aidha, kila idara imeanzisha kitengo cha ufilisi kwa waliojipatia mali kwa uhalifu ikiwa ni baada ya mahakama kutoa hukumu za kesi za uhujumu uchumi.

Habari Kubwa