DPP aiondoa rufani dhidi ya Mramba, Yona

22Jun 2016
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
DPP aiondoa rufani dhidi ya Mramba, Yona

MKURUGENZI wa Mashitaka nchini (DPP), ameiondoa mahakamani rufani aliyoikata dhidi ya mawaziri waandamizi wa zamani wa Fedha, Basil Mramba na wa Niashati na Madini, Daniel Yona iliyopangwa kusikilizwa jana katika Mahakama ya Rufani Tanzania.

Rufani hiyo iliondolewa jana kabla ya kuanza kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Mbarouk Mbarouk, Salum Massati na Profesa Ibrahim Juma.

Juni 20, mwaka huu, DPP aliwasilisha kusudio la kuondoa rufani hiyo chini ya kanuni ya 77(1) ya Mahakama ya Rufani pamoja na nakala kukabidhiwa kwa mawakili wa utetezi.

Hata hivyo, jopo hilo lilisema kwamba kifungu alichokitumia DPP kuwasilisha kusudio hiyo siyo sahihi kwa kuwa kinatumika kabla ya shauri halijapangwa kusikilizwa.

Jaji Mbarouk alisema DPP alitakiwa kutumia kanuni ya 4(2)(a) ya Mahakama ya Rufani kuomba kuondoa rufani hiyo.

Mawakili wa Serikali Waandamizi, Theophil Mutakyawa na Shadrack Kimaro, walieleza nia ya DPP ya kuondoa rufani hiyo, jambo ambalo halikuwa na pingamizi kwa upande mwingine.

Jopo hilo lilikubali maombi ya kuondoa rufani hiyo.

Awali, mahakamani hapo, DPP alikata rufani kupinga hukumu iliyotolewa Oktoba 2, mwaka 2015 na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam iliyoketi chini ya Jaji Projest Rugazia.

Jaji Rugazia alisema mawaziri hao walitakiwa kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili na siyo miaka mitatu kama Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilivyowahukumu dhidi ya mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka.

Kadhalika, Jaji Rugazia alikubaliana na hukumu ya kumuachia huru Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja.

Hata hivyo, DPP alikata rufani Mahakama Kuu, kupinga adhabu waliyopewa mawaziri hao wa zamani kwamba ni ndogo kwa sababu jopo la mahakimu watatu waliotoa hukumu hiyo walikosea kumuachia huru Mgonja.

Mbali na kupinga adhabu hiyo, DPP aliomba mahakama kuwaamuru washtakiwa kulipa fidia ya fedha walizosababisha hasara.

Mahakama ya Kisutu iliwahukumu Mramba na Yona kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa faini ya Sh. milioni tano baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7 kutokana na kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni ya kukagua madini ya dhahabu ya M/S Alex Stewart ya Uingereza.

Kwa sasa mawaziri hao wanatumikia kifungo cha nje baada ya kupendekezwa kuwa miongoni mwa wafungwa wanaohitaji kumalizia sehemu ya kifungo chao wakiwa nje, ikiwamo kufanya usafi katika Hospitali ya Sinza Palestina.

Habari Kubwa