DPP akabidhi serikali kilo 325 za dhahabu zilizotoroshwa

01Jun 2019
Rose Jacob
MWANZA
Nipashe
DPP akabidhi serikali kilo 325 za dhahabu zilizotoroshwa

HATIMAYE dhahabu kilo 319.59 yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 27 na Sh. milioni 305 zilizokamatwa wilayani Sengerema kati ya Januari 4 na 5, mwaka huu mkoani Mwanza, zimekabidhiwa Wizara ya Fedha na Mipango na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kutokana na kutokuwapo kwa rufani dhidi ya watuhumiwa.

Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Biswalo Mganga.

Dhahabu hiyo ilidaiwa kutoroshwa kwa njia ya panya kwa lengo la kukwepa kodi na kilo tano zilizoshindwa kulipiwa kodi mkoani Geita.

Tangu ilipokamatwa iliwekwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), tawi la Mwanza kwa ajili ya usalama.

 DPP alikabidhi dhahabu hiyo kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Khatibu Kazungu, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dotto James, ili kuhakikisha mipango thabiti ya maendeleo inafanyika na kuleta tija ndani ya jamii na nchi kwa ujumla.

Akizungumza katika makabidhiano hayo yaliyofanyika  BoT tawi la Mwanza, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Biswalo Mganga, alisema baada ya mahakama kutoa hukumu katika kesi namba moja ya mwaka 2019 ya uhujumu uchumi dhidi ya washtakiwa wanne ambao ni Sajid Abdallah, Kisabo Kija, Emmanuel Kidaya na Hassan Sadick, wanaodaiwa kutenda kosa la kuwapatia rushwa ya Sh. milioni 700 watuhumiwa wanne ambao ni askari polisi ili kuwasaidia kutorosha madini hayo, kushindwa kukata rufani.

Watuhumiwa hao walihukumiwa kwenda jela miaka 15  kila mmoja au kulipa faini ya Sh. milioni 529, ikiwamo kutaifisha mali zote zilizo husika katika utoroshaji wa madini hayo. Washtakiwa hao walilipa faini na kuwa huru.

"Tangu Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, Roda Ngimilanga, alipotoa hukumu dhidi ya watuhumiwa hao ambao ni wafanyabiashara wa madini Machi 23, mwaka huu, tulisubiri kama watakata rufani, lakini mpaka sasa hakuna kilicho tendeka hivyo mali hii imekuwa ni halali kwa serikali na leo (jana) ninaikabidhi Wizara ya Fedha kilo 325.31 za dhahabu na fedha kiasi cha Sh. milioni 305,"alisema Biswalo.

Aidha, Biswalo aliikabidhi wizara hiyo mashine moja ya kupimia ubora wa dhahabu, mizani mbili za kupimia uzito wa dhahabu, magari mawili, Toyota KLUGGER lenye namba za usajili T 726 DPJ na Toyota Mark II T208 DLT.

Biswalo alisema dhahabu kilo 5.72 zilizokamatwa zinafikisha idadi ya kilo 325.31 zenye thamani ya Sh. milioni 394, ambazo zilitakiwa kulipiwa kodi Sh. milioni 27, zilikamatwa mkoani Geita zikisafirishwa na raia wa kigeni wa Afrika Kusini, Baarend Van Brakel, mnamo Oktoba 29, mwaka jana.

Waziri wa Madini, Dotto Biteko, ambaye alikuwapo kushuhudia makabidhiano hayo, aliwataka wananchi na wafanyabishara kuepuka hasara kwa kulipa kodi.

"Hawa watu wamekwepa kulipa kodi ya bilioni moja angalia leo wamepoteza fedha nyingi zaidi ya bilioni 27 ambazo zingeongeza tija kwao na kuwa wawekezaji wakubwa, serikali haifurahii masuala haya kwa wananchi wake fedha hizi zingewasaidia katika mitaji, lakini wamezipoteza kwa uzembe,” alisema Biteko.

Aidha makabidhiano hayo yalihudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na kamati yake ya ulinzi na usalama na Mkuu wa Wilaya husika ya Nyamagana, Dk. Phills Nyimbi.

Habari Kubwa