DPP aomba kutaifishwa nyumba za mshtakiwa

14Nov 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
DPP aomba kutaifishwa nyumba za mshtakiwa

MKURUGENZI wa Mashtaka nchini (DPP), amewasilisha maombi Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Uhujumu Uchumi na Rushwa, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi, kutaka kutaifisha mali zikiwamo nyumba 7 za mke wa aliyekuwa miongoni mwa Wakurugenzi wa Kampuni ya Superior Financing Solutions, ...

Aloysius Gonzaga, Magreth Gonzaga.

Maombi hayo namba 1/2019 yanatarajia kuanza kusikilizwa mbele ya Jaji Sirilius Matupa, Novemba 26, mwaka huu.

Katika maombi hayo, DPP anaomba kutaifisha ploti namba 199, Block D, namba 121302 iliyoko Tegeta, Ploti namba 200 Block D namba 39021 iliyoko Tegeta.

Zingine ni ploti namba 1378, Block, E Tegeta ikiwa namba za hati 41275 na ploti namba 176 Block B iliyoko Aman Gomvu ikiwa na hati namba 138598, ploti namba 191, Block B iliyoko Aman Gomvu ikiwa na hati namba 132797 na namba 174 Block B iliyoko Aman Gomvu ikiwa na hati namba 138597.

Mapema mwaka huu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilitangaza kumsaka Magreth anayedaiwa kumiliki nyumba tatu za kifahari jijini Dar es Salaam huku akituhumiwa kutakatisha fedha haramu kinyume cha Kifungu Na. 12(d) na 13(a) cha Sheria ya Utakatishaji Fedha Haramu Na. 12 ya Mwaka 2006.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru (wakati huo), Diwani Athumani, alisema wanamsaka Magreth kupitia tangazo lililotolewa kwa amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inayosikiliza shauri la jinai namba 28 la mwaka 2019.

Alidai Gonzaga ambaye kwa sasa anadaiwa kukimbilia nje ya nchi, anatafutwa na Takukuru kwa tuhuma za kutakatisha fedha haramu na kujipatia mali kupitia Superior Financing Solution Limited (SFS) inayodaiwa kufanya biashara bila kulipa kodi ya serikali.

Gonzaga na mwenzake Isaack Kasanga wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 5/2019 katika Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 45 ambayo ni kula njama, kutenda kosa moja, kughushi (12), kuwasilisha nyaraka za uongo (tisa), kushindwa kulipa kodi na utakatishaji fedha mashtaka 30.

Inadaiwa kati ya Machi 2, 2010 na Aprili 26, 2016 katika maeneo tofauti ndani ya Jiji la Dar es Salaam washtakiwa hao walikula njama kwa kughushi, kukwepa kulipa kodi na kutakatisha.

Habari Kubwa