DPP Z’bar afunguka makosa ya udhalilishaji

11Mar 2017
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
DPP Z’bar afunguka makosa ya udhalilishaji

MKURUGENZI wa Mashtaka Zanzibar, Mzee Ibrahim Mzee, amesema makosa ya udhalilishaji Zanzibar yanaongezeka kwa kasi na kwamba watoto wengi wadogo chini ya miaka 18 wa kike na wakiume wanafanyiwa matendo hayo.

MKURUGENZI wa Mashtaka Zanzibar, Mzee Ibrahim Mzee.

Akizungumza na Nipashe, alisema takwimu za vitendo hivyo vinaonesha kuwa hali inazidi kuwa mbaya na kueleza kuwa tayari vyombo vinavyohusika vimeshakaa na kutafakari kwa kina kuhusu ongezeko hilo na wameamua kuanzisha operesheni maalumu ya kushughulikia kesi hizo.

Alisema kutokana na hali ilivyo kwa sasa, ni vyema mahakama zisitoe dhamana kwa watuhumiwa wa kesi za udhalilishaji. Mzee alisema kumekuwapo na malalamiko mengi kutoka kwa jamii kuhusiana na uendeshaji wa kesi za udhalilishaji.

“Huko nyuma ni kweli tumekuwa tukipata matatizo hayo na mengi ya hayo, wengine wanasema matatizo ya kisheria na vyombo vyenyewe vya maamuzi, lakini kwa wanaosema tatizo ni sheria kesi nyingi za udhalilishaji zinapelekwa mahakama ya mkoa na mahakama ya mkoa adhabu yake ni miaka saba, lakini tumekuwa na baadhi ya mahakimu sio waadilifu na kesi za udhalilishaji kushindwa kutolewa adhabu stahiki,” alisema DPP.

Alisema mambo hayo yamekuwa yakiwavunja moyo wanajamii na wakati mwingine kupelekea wananchi wasijitokeze katika kutoa ushahidi mahakamani kuhusiana na kesi hizo.

Aidha, DPP huyo alisema wanatekeleza mradi wa marekebisho ya sekta ya sheria Zanzibar ili kuzifanyia mapitio sheria za msingi zinazohusiana na makosa ya jinai ikiwamo sheria ya ushahidi ambayo ni ya muda mrefu, sheria ya adhabu ya mwaka 2004 na sheria ya mwenendo wa jinai ya mwaka 2004 na tayari ziko katika mchakato wa kufanyiwa marekebisho.

Habari Kubwa