EAC yajipanga kukabiliana na majanga

17May 2019
Na Mwandishi Wetu
GENEVA
Nipashe
EAC yajipanga kukabiliana na majanga

NCHI za Afrika Mashariki (EAC), zimewasilisha mapendekezo tisa kwenye mkutano wa dunia wa wadau kujadili utekelezaji wa mkataba wa kupambana na majanga duniani uitwao Sendai.

Mtaalamu wa Mabadiliko ya Tabianchi wa EAC, Dismas Mwikila.

Mkataba wa Sendai ulisainiwa na nchi mbalimbali duniani Tanzania ikiwamo mwaka 2015 nchini Japan, na kufuatiliwa na tamko la pamoja la Tunisia.

Utekelezaji wa mkataba huo ambao utaenda hadi mwaka 2030, una lengo la kuongeza jitihada za kukabiliana na majanga ya asili na yanayosababishwa na binadamu yanayotokea duniani kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Majana hayo ni tetemeko la ardhi, magonjwa, njaa, ukame kupindukia, mafuriko, mvua nyingi, mabadiliko ya vipindi vya mvua, maporomoko ya ardhi na miamba na kuongezeka kwa kina cha bahari huku sehemu ya ardhi ikimezwa.

Mkataba wa Sendai una malengo manne na vipaumbele saba, kwa wadau wa serikali, sekta binafsi, vyombo vya habari, makundi maalum na wananchi kuweka juhudi za pamoja katika kupunguza athari zinazosababishwa na majanga.

Akizungumza na Nipashe jijini Geneva, Uswis, Mtaalamu wa Mabadiliko ya Tabianchi wa EAC, Dismas Mwikila, alisema majanga yanapotokea kuna kuwa na athari kubwa za kiuchumi kwa nchi husika kwa watu kufariki, kujeruhiwa na uharibifu mkubwa wa miundombinu.

Alisema athari nyingine ni watu kukosa makazi baada ya mafuriko kuharibu nyumba na mali zao nyingine, magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.

“Hivi karibuni tumeona kilichotokea Msumbiji na Malawi ilikuwa ni janga kubwa kutokana na kimbunga ambacho ni matokeo ya mabadiliko ya tabianchi. Mkataba wa Sendai unataka kuwa na mkakati wa kukabiliana na matokeo ya majanga kwa kujiandaa vyema,” alisema.

Alitaja mapendekezo hayo ni kuzijengea uwezo taasisi ikiwamo Mamlaka za hali ya hewa za nchi husika, kuwa na tekonolojia ya kutabiri karibu na usahihi majanga kabla na kusambaza taarifa kwa wananchi.

Alisema pia kuwa na sera pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa mkataba huo kuanzia ngazi ya jamii ambako kuna waathirika wa majanga husika.

Alisema kuimarisha mpango wa kukabiliana na majanga kwa kila nchi, kuwa na utaratibu wa kutoa taarifa na data za kabla ya janga kutokea kutolewa na mamlaka ya hali ya hewa.

Jingine ni kuyajengea uwezo makundi ya wanasayansi na wataalamu wa teknolojia, vijana, asasi na sekta binafsi ikiwamo kushirikiana nchi moja na nyingine kwa majanga yanayoweza kutokea na kuhusisha nchi zaidi ya moja kwa wakati mmoja, kwa kuwa na mpango shirikishi.

Mwikila alisema eneo jingine ni kuwekeza kwenye kujenga uwezo wa kisayansi na teknolojia kwa vyuo vikuu, vyuo vya mafunzo ya ufundi ikiwamo shule za msingi na sekondari kwa kuwa na uelewa wa kukabiliana na majanga.

Alisema EAC imeridhia mkataba huo na kuupitisha kwa ajili ya utekelezaji wa nchi wanachama, kwa kuwa ndani yake kuna malengo manne yanayopaswa kutekelezwa ifikapo 2020.

Mkutano huo ulioitishwa na Umoja wa Mataifa kupitia shirika la kukabiliana na majanga duniani (UNDRR), umewaleta pamoja wadau zaidi ya 500 kutoka nchi mbalimbali duniani, ikiwamo wanawake, walemavu, asasi za kiraia, serikali na vyombo vya habari.

Habari Kubwa