EAC yatenga dola 25,000 mashindano wanafunzi vyuo vikuu

02Dec 2019
Daniel Sabuni
ARUSHA
Nipashe
EAC yatenga dola 25,000 mashindano wanafunzi vyuo vikuu

JUMLA ya Dola 25,000 zimetengwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa ajili ya mashindano ya wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka kwa nchi wanachama watakaotengeneza video inayohusu mafanikio na shughuli za zinazofanywa na jumuiya hiyo.

Baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiadhimisha miaka 20 Tangu kuanzishwa EAC, Picha na Daniel Sabuni.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika mashariki Balozi Liberat Mfumukeko, amesema hayo leo wakati akiongea na waandishi wa habari na wanafunzi wa vyuo mbali mbali wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki waliofiki kuadhimisha kilele cha miaka 20 ya Jumuiya hiyo yanayofanyika Makao Makuu ya EAC.

Amesema pesa hizo ambazo zimelengwa kuunganisha vijana wa nchi sita wanachama wa Jumuiya lakini pia kueneza uelewa kwa shughuli na mafanikio yaliyofikiwa kwa miaka 20 tangu kuzaliwa kwa EAC ili kuwa na nguvu moja kiuchumi lakini pia kupunguza umaskini kwa wananchi wake.

“Washindi 30 ambao watatengeneza video ambazo zitagusa vigezo watafaidika na pesa hizo, video inatakiwa iwe na sekunde 30 hadi 45 kuoyesha EAC imefanya nini, hili litahusisha watu takribani milioni 10”amesema….Video hizo moja ya kigezo ni kuziweka kwenye mitandao ya kijamii ambayo inafikiwa na watu wengi .

Amesema Lengo la EAC ni kuwaunganisha vijana ambao ni kundi kubwa zaidi lenye nguvu na chachu ambao mbali na kufaidika na Jumuiya lakini pia ni wepesi kuelezea mafanikio, adhma ya na malengo kwa makundi mengine ili hatimaye kuunganisha Nchi zetu sita katika kila Sekta ili kuleta maendeeo ya kweli na kufikia uchumi wa kati kwa ngazi ya kaya.

Aidha, amesema adhimisho la miaka 20 ya Jumuiya pia limelenga kuhakikisha elimu inakuwa na ubora kwa nchi zote na ndo maana hukutanisha wanafunzi, wataalamu ili kubadilishana uzoefu ili kuboresha upande wenye udhaifu.

Huku lengo linguine likitajwa kuwa ni kuwaunganisha vijana wa Jumuiya ambao ni asilimia 65 ya wananchi wa nchi zote ni kuona nguvu ya vijana katika ushawishi lakini pia kutumia jukwaa la elimu kupitia vyuo kama wasomi ili kueneza fursa za kimaendeleo kama ajira ujasiriamali na biashara za pamoja kwa ujumla.

Ameongeza kuwa EAC imekuwa ikiweka mkazo na kuwezesha suala la viwanda kwa nchi wanachama ili kuwa na viwanda vingi ambavyo vitapunguza changamoto za ajira kwa vijana na wananchi wengine.

Amesema pia EAC imewezesha kujengwa kwa Hospitali ya kitengo cha moyo jijini Dar es salaam katika Hospitali ya Muhimbili Nchini Tanzania na pia Hospitali ya matibabu ya figo nchini Kenya ili kupunguza safari za wagonjwa waliokuwa wakisafiri umbali mrefu kwenda nchi za nje kutafuta matibabu na hivyo kupunguza gharama.

Amesema Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) imekuwa nguzo kwa maendeleo ya jumuiya kwani imekuwa nguzo ya mikopo ya masharti nafuu kwa miradi mbali mbali ya nchi wanachama ambapo EAC imekuwa ikiwezesha Nchi hizo kupata mikopo.

Habari Kubwa