Elimu kupinga ukatili wa kijinsia yatolewa Kigoma Ujiji

03Dec 2021
Adela Madyane
Kigoma
Nipashe
Elimu kupinga ukatili wa kijinsia yatolewa Kigoma Ujiji

MANISPAA ya Kigoma Ujiji imetoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa kuwajengea uwezo mabaraza ya usuluhishi ya migogoro katika ngazi ya kata kwa lengo la kupambana na vitendo hivyo.

washiriki wa baraza la usuluhishi katika kata ya Buzebazeba iliyoko MANISPAA YA Kigoma UJIJI WAKIWA KATIKA PICHA YA PAMOJA baada ya mafunzo ya kupinga ukatili wa kijinsia YALIYOTOLEWA LEO. PICHA ADELA MADYANE.

Elimu hiyo inayotolewa kwa ufadhili wa BAKAID wa kupambana na kupinga ukatili wa kijinsia chini ya Shirika la Norwegian Church Aid (NCA) imetolewa kwa kata za Kipampa, Buzebazeba, Rusimbi na Majengo.

Elimu hiyo imetolewa na wataalamu wa maendeleo ya jamii, ustawi wa jamii, maafisa wa jeshi la polisi dawati la jinsia, wasaidizi wa kisheria na viongozi wa dini.

Afisa maendeleo ya Jamii katika manispaa hiyo, Jabir Majira, ameyataka mabaraza ya usuluhishi wa migogoro ngazi ya kata kuendelea kutatua changamoto za ukatili ambazo zimekuwa zikijitokeza kwa kutoa elimu katika mikutano ya Wananchi na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu kwa kupinga vitendo vya ubakaji, kuwatumikisha watoto kazi ngumu, kutowapeleka watoto shule na unyanyasaji wa kuwanyima fursa wanawake kujiingizia kipato.

Mkaguzi msaidizi wa jeshi la polisi dawati la jinsia, Anastasia Daudi, ameyataka mabaaraza hayo kuelimisha jamii kusimamia malezi ya familia na kuripoti vitendo vya ukatili vinavyojitokeza na kutoa ushirikiano katika kushughulikia vitendo hivyo, kwa uongozi na viongozi wa mtaa, kata, ustawi wa jamii na jeshi la polisi.

Naye, afisa mradi wa kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kutoka BAKAID Kigoma, Juma Bewa, amewataka maafisa watendaji kata na mtaa kuhakikisha katika vikao na mikutano ya wananchi wanatoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili kila mara na kuweka kauli mbiu ya eneo husika ya kupinga vitendo hivyo ili jamii zipate kuwa salama.

Habari Kubwa