Elimu ya madhara ya ukatili kingono vyuoni

06Dec 2018
Frank Monyo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Elimu ya madhara ya ukatili kingono vyuoni

MFUKO wa Ruzuku wa Uwezeshaji Vituo vya Msaada wa Kisheria (LSF), unatarajia kuanzisha mpango wa kuvifikia vyuo vya elimu ya juu nchini kwa lengo la kutoa elimu juu ya madhara ya ukatili wa kingono kwa wanafunzi na wakufunzi.

Mkurugenzi Mtendaji wa LSF, Kees Groenendijk akizungumza na waandishi wa habari juu ya uinduzi wa kampeni hiyo.

Mpango huo utaanza zikiwa siku chache baada ya Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Vicensia Shule, kufichua kukithiri kwa rushwa ya ngono chuoni hapo.

Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Miradi wa LSF, Scholastica Jullu, baada ya kuzinduliwa kwa kampeni ya "Siyo Tatizo Tena" yenye lengo la kuongeza ufahamu kwa jamii kuhusu uwapo na upatikanaji wa huduma za bure za misaada ya kisheria kwa wananchi hasa wanawake unaotolewa na wasaidizi wa kisheria.

Jullu alisema kampeni hiyo itafanyika kwa miezi sita katika wilaya zote nchini kuanzia sasa na kuwataka Watanzania wenye matatizo ya kisheria kujitokeza kuomba msaada wa kisheria kwa wasaidizi wa sheria ambao watawasaidia kuyatatua matatizo yao au kuwaeleza pa kuyapeleka.

"Sisi hatuangalii huo ukatili ambao unaojitokeza katika vyuo vikuu...kuna taasisi mbalimbali ambazo tunazifadhili za watoa msaada wa sheria ambazo zinashughulika na kutoa elimu juu ya unyanyasaji wa kijinsia,” alisema.

"Hata sisi (LSF) tuna mpango wa kufika katika hivyo vyuo kuelewesha wanafunzi pamoja na wakufunzi wao jinsi gani huo ukatili unaweza kukuletea madhara...kwa sababu unapata hizo maksi za bure, lakini kwenye utendaji ukija kwenye mashirika kama haya ya kwetu hutofanya vizuri,” aliongeza Jullu.

Jullu alisema LSF inajivunia mafanikio kwa kuwa katika wilaya zote hivi sasa kuna wasaidizi wa kisheria 25, ambapo kwa mwaka 2017 wamewafikia watu milioni 1.5 na kwa mwaka 2018 wamewafikia watu milioni 2.5 ambao wamepatiwa elimu na kuzifahamu haki zao.

Kwa upande wa msaada wa kisheria wa mtu mmoja mmoja, wamewafikia watu 67,000 na kuwafanya wananchi wengi kuishi kwa amani na zoezi lote hilo limefanyika bila gharama.

Alisema wasaidizi wa kisheria wanasaidia kutoa elimu kwa wananchi ili wa zifahamu sheria na kuzitumia na kwa kushirikiana na serikali na kuwa mafunzo ya wasaidizi ya sheria waliopewa siku za nyuma wamejengewa uwezo, ili kufanya kazi zao vizuri kwa kufuata matakwa ya sheria mpya ya 2017.

Awali akizindua kampeni hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa LSF, Kees Groenendijk, alisema pia italeta unafuu zaidi hasa kwa wanawake wenye hali ngumu ambao haki zao za msingi zimekuwa zikiminywa.

"LSF Tanzania inaendelea kuwezesha upatikanaji wa huduma hizi za usaidizi wa kisheria bure kwa wananchi bila gharama yoyote na imejikita zaidi kusaidia jamii ya watu mbalimbali hasa wa hali ya chini kiuchumi," alisema Groenendijk.

Habari Kubwa