EU, Haki za Binadamu walaani shambulio dhidi ya Tundu Lissu

09Sep 2017
Mary Geofrey
Nipashe
EU, Haki za Binadamu walaani shambulio dhidi ya Tundu Lissu

SIKU moja baada ya Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, kushambuliwa na kujeruhiwa katika sehemu mbalimbali za mwili wake, Umoja wa Ulaya (EU) umelaani tukio hilo.

Lissu, ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) na Mbunge wa Singida Mashariki, alijeruhiwa kwa risasi maeneo ya mikononi, miguuni na tumboni na yuko Nairobi, Kenya kwa ajili ya matibabu.

“Kwa ushirikiano na mabalozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, wenye uwakilishi Tanzania, Umoja wa Ulaya, tunaungana na Serikali ya Tanzania, Bunge na mashirika ya kiraia kulaani vikali jaribio lililohatarisha maisha ya Tundu Lissu,” ilieleza taarifa hiyo ya EU.

 Jumuiya hiyo pia imevitaka vyombo vya dola kuwachukulia hatua wale wote waliohusika na tukio  hilo na kwamba wanamwombea apone haraka.

Mbali na EU, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) nayo imekemea tukio hilo, ililoliita ni uvunjifu wa sheria na haki za binadamu.

Mwenyekiti wa THBUB, Bahame  Nyanduga, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, alieleza kuwa tukio hilo si la kawaida na limeleta hofu kwa ya familia ya Tundu Lissu na Watanzania.

“Isitoshe, matukio haya hayaleti picha nzuri kwa nchi inayoheshimu demokrasia, haki za binadamu na utawala bora. Hivyo, THBUB, inalitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linakamilisha haraka upelelezi wa tukio hilo na kuwapeleka wahusika katika vyombo vya sheria,” alisema.

Pia Baraza la Uongozi wa TLS, nalo lilitoa taarifa ya kulaani na kukemea tukio hilo na kuvitaka vyombo vya dola kuingilia kati ili kuwapata wahalifu waliohusika.

Makamu wa Rais wa TLS, Godwin Ngwilimi, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari alieleza kuwa wanafuatilia kwa karibu tukio hilo kwa ajili ya kutoa taarifa na kuwata wanachama wote kuwa watulivu.

Habari Kubwa