Ewura kuanzisha vituo vya mafuta vinavyotembea

26Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Njombe
Nipashe
Ewura kuanzisha vituo vya mafuta vinavyotembea

MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati, Maji na Mafuta nchini (Ewura), imesema inatarajia kuanzisha huduma ya vituo vya mafuta vinavyotembea (mobile pump station) kwa kutumia magari maalumu yaliyotengenezwa kwa kazi hiyo, zikiwamo pikipiki za miguu mitatu ambazo zinaendelea kuundwa kupitia Chuo cha (UDSM).

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa ewura Titus Kaguo, picha mtandao.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa mamlaka hiyo, Titus Kaguo, wakati akijibu maswali ya baadhi ya wadau wa Ewura walioshiriki katika mkutano uliofanyika mjini Njombe, uliokuwa na lengo la kutoa elimu ya msingi ya udhibiti wa nishati mafuta na maji pamoja na kutambulisha ofisi mpya ya kanda, uliofanyika mkoani Njombe.

Kaguo alisema hatua hiyo itarahisisha upatikanaji wa nishati ya mafuta na kusisitiza kuwa nishati ya mafuta inatakiwa kuuzwa kwa utaratibu unaokubalika na kwa kuwa kujenga visima vikubwa ni gharama, wameona njia hiyo ni bora na itakuwa ni rahisi kuwafikia wateja wengi.

Alisema katika maeneo mengi hapa nchini, wafanyabiashara wadogo wamekuwa wakisafirisha na kuuza mafuta kwa njia ambazo sio sahihi na zinazohatarisha usalama wa vyombo vya watumiaji pamoja na maisha yao na kuchukulia mfano hasa maeneo ya vijijini ambako hakuna vituo vya mafuta.

“Hata hivyo, Ewura tumejitahidi kukomesha tatizo la uchakachuaji wa mafuta ambalo lilikuwa limekithiri siku chache zilizipita, lakini sasa limekwisha baada ya kutumia njia ya vinasaba vya rangi pamoja kwa kupitia uagizaji wa mafuta kwa pamoja katika meli moja,” alisema Kaguo.

Kaguo pia alishauri watumiaji vya vyombo vya moto kuacha kujaza mafuta katika vyombo vyao wakati wa mchana kwa kuwa kiasi fulani cha mafuta hupotea kwa njia ya mvuke na kusababisha malalamiko ya kupunjwa mafuta na wahudumu au wamiliki wa vituo.

Aliongeza kuwa watu wanatakiwa kufahamu kuwa kusafirisha kuuza mafuta kwa njia zisizo rasmi kwa kutumia madumu ni kosa kisheria na pia hatari inayoweza kusababisha majanga kama milipiko ya moto.

“Kutokana na ongezeko la vyombo vya usafiri kama pikipiki, tumeamua kupunguza gharama za kuanzisha vituo vya uuzaji mafuta ili viweze kujengwa katika maeneo mbalimbali hasa vijijini ili kuepuka uuzaji mafuta katika vidumu,” alisema Kaguo.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka, aliwapongeza Ewura kwa kuanzisha ofisi za kanda ambazo zitahudumu mikoa ya Njombe, Ruvuma, Mbeya na Katavi kwa kuwa wamesogeza huduma karibu na wakazi wa mikoa hiyo na kurahisisha uwasilishaji wa changamoto zao katika ofisi husika na kupatiwa ufumbuzi kwa haraka badala ya kusubiri changamoto zao kutatuliwa makao makuu, jijini Dar es Salaam.

Habari Kubwa