EWURA yafichua wenye magari wanavyoibiwa mafuta

27Nov 2020
Joseph Mwendapole
Dar es Salaam
Nipashe
EWURA yafichua wenye magari wanavyoibiwa mafuta

MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) imefichua jinsi wenye magari wanavyoibiwa na watumishi wa vituo vya mafuta wanapokwenda kujaza mafuta.

Imesema ili kuepuka hali hiyo ni vyema wenye magari wadai risiti kila wanapojaziwa mafuta na pia kushuka kwenye magari yao ili kuhakiki kwa makini mafuta yanavyojazwa.

Meneja Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo, alisema hayo wakati wa mkutano na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari.

Alisema mtu anapokwenda kujaza mafuta anapaswa kuhakikisha kwenye pampu inasomeka alama 00 ndipo aanze kujaziwa mafuta, vinginevyo anaweza kuibiwa.

“Mfano kama kuna mtu kapita hapo kajaza mafuta ya 20,000 na wewe umepita unataka kujaza pengine 50,000 hakikisha alama zile kwenye pampu zinasomeka ‘00’ kwa sababu usipohakiki utajaziwa kwa kuanzia ile 20,000 aliyojaziwa mwenzako,” alisema.

Alisema ili kuepuka usumbufu kama huo ni vyema wenye magari wakaachana na kawaida ya kubaki kwenye magari wakiendelea na mambo mengine kwa kuwa hali hiyo inatoa mwanya wa kuibiwa na watumishi wa aina hiyo.

Alisema ili uanze kujaziwa mafuta hakikisha mkono wa pampu umerudi kwenye sehemu yake ya kawaida na hesabu isome 00.

“Kama mkono wa pampu haujarudi kwenye sehemu yake ya kawaida inamaana akikuwekea mafuta unaweza kukuta hesabu inaanzia ile ambayo mwenzako aliyepita amewekewa,” alisema.

Mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Deodatus Balile, alisema kuna baadhi ya pampu kwenye vituo vya mafuta ambazo zimechoka na haziwezi kukaa kwenye nafasi yake ya kawaida baada ya kuweka mafuta.

Alisema hali hiyo imesababisha watu wengi wenye magari kuibiwa mafuta na baadhi ya watumishi wa vituo vya mafuta bila kujua wanapokwenda kujaza.

Akizungumzia tatizo hilo, Kaguo alisema Wakala wa Vipimo (WMA), imekuwa ikifanya ukaguzi wa pampu hizo mara kwa mara kuhakikisha watumiaji hawaibiwi, lakini wanunuzi wa mafuta nao wanapaswa kuwa waangalifu.

“WMA wanafanya ukaguzi kama zile pampu zinapitisha mafuta kwa kiwango kile kile lakini wizi mkubwa huwa unafanyika kwa njia niliyoitaja awali,” alisema.

Kaimu Mkurugenzi wa Ewura, Godfrey Chibulunje, aliwataka Watanzania kuacha kutumia mafundi umeme wasiosajiliwa na mamlaka hiyo ili kuepuka uwezekano wa kupata hasara ya kuunguliwa na nyumba zao.

Alisema mamlaka hiyo inawasajili mafundi umeme waliokidhi vigezo vya kufanyakazi hiyo, hivyo hakuna haja ya kutumia wa mitaani wasio na sifa.

“Ukiingia kwenye kanzidata yetu utakuta orodha ya mafundi ambao tayari tumewasajili kwa hiyo akija mtu anataka kukufanyia kazi chukua leseni yake na uchungulie kwenye kanzidata yetu yupo au la,” alisema.

Alisema kuna baadhi ya tuhuma zinatolewa kuwa baadhi ya wanafunzi huingia shuleni na simu na kwenda kuzichaji kinyemela darini.

“Kuna tetesi kwamba kwa sababu wanafunzi hawaruhusiwi kwenda na simu shuleni ukifika muda wa kuchaji wanapanda darini kuzichaji sasa huko wanakata nyaya wanavyojua wao jambo ambalo linadhaniwa limekuwa likisababisha moto kwenye baadhi ya shule,” alisema.

Pia, alisema Watanzania wanapaswa kujenga utamaduni wa kufanya ukaguzi wa mifumo ya umeme kwenye nyumba zao kila mwaka ili kuhakikisha kama imekaa sawa ili kuzuia ajali za moto.

Habari Kubwa