Faida, hasara Tanzania kuingia uchumi wa kati

03Jul 2020
Na Waandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Faida, hasara Tanzania kuingia uchumi wa kati

WAKATI serikali ikitaja mambo 10 yaliyochangia Tanzania kuingia katika kipato cha kati kwa kundi la chini mwaka 2020, wataalamu wa uchumi wameeleza faida na hasara za kuingia kwenye orodha hiyo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, kuhusu mambo mbalimbali ikiwa pamoja na sababu zilizoifanya Tanzania kutangazwa na Benki ya Dunia kuwa imeingia katika orodha ya nchi zenye uchumi wa kati. PICHA: PAUL MABEJA

Juzi, Benki ya Dunia iliitangaza Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zilizofikia uchumi wa kati kwa kundi hilo ikiwa ni miaka mitano kabla ya lengo la Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 iliyoandaliwa mwaka 1999.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma jana, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi, alisema Tanzania ilipaswa kufikia hatua hiyo miaka mitano ijayo.

Alifafanua kuwa katika Benki hiyo kuna mgawanyo wa makundi matatu kulingana na viwango vyao vya uchumi na Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu pekee za Afrika zilizoingia kwenye kundi la kipato cha kati juzi na imekuwa nchi ya pili kwa Afrika Mashariki.

“Hatua hii imeakisi azma ya Rais John Magufuli ya kuwa sisi si nchi maskini, uchumi wa kati unamaanisha nchi imetoka katika umaskini na kuwa matajiri, lakini siyo sana,” alisema.

Dk. Abbasi aliyataja mambo 10 yaliyoibeba Tanzania kuwa ni pamoja na kuwekeza kwenye miradi ya kimkakati na kufanya uamuzi mgumu.

Mengine ni Amani na utulivu, mipango thabiti ya maendeleo, utekelezaji usioyumba, azma ya kujitegemea, nidhamu katika matumizi, kuimarisha miiko ya viongozi, kuwekeza katika maendeleo ya watu na sekta binafsi yenye tija.

Alibainisha kuwa dira inakazia kuwa, ili kufikia uchumi wa kati, ni lazima kuwa na uchumi imara na uchumi wa kipato cha kati uwe umewekezwa kwenye viwanda jambo ambalo limefanyika na kwa kipindi cha miaka mitano, vipo zaidi ya 8,000 vilivyoanzishwa, kujengwa na vingine vinamaliziwa.

Dk. Abbasi alisema viongozi wa serikali za awamu zote wamechangia kufikia hatua hiyo, akisisitiza kuwa uwekezaji katika miradi ya kimkakati ikiwamo ujenzi wa reli ya kisasa, imechangia kwa kiwango kikubwa.

“Kama kuna kitu kimechagiza sana ni uamuzi wa serikali wa kuwekeza kwenye miradi ya kimkakati, leo Tanzania inatekeleza miradi ambayo wengine wananuna, viwanda vimejengwa,” alisema.

Alisema kuna wakati serikali zote zimefanya uamuzi mgumu hadi kusababisha kutungiwa majina ikiwamo udikteta.

FAIDA NA HASARA

Wakati serikali ikiyasema hayo, watalaamu wa uchumi wamebainisha faida na hasara kwa Tanzania kuingia katika uchumi huo.

Katika mazungumzo na Nipashe jana, mchumi Junior Ndesanjo alisema dhana ya nchi kuingia katika uchumi wa kati ina maana kwamba pato la mwananchi limekua na thamani ya bidhaa kwenye masoko imeongezeka.

“Uchumi wa kati juu (kipato cha mwananchi) ni Dola za Marekani 4,000 na uchumi wa kati chini ambayo Tanzania tumeingia humo ni kuanzia Dola 1,036 (Sh. milioni mbili) kwa mwaka, siyo kila Mtanzania anapato hilo, bali ni pato la wastani,” alifafanua.

Ndesanjo alisema uchumi wa kati wa chini unalitambulisha taifa kimataifa, hivyo kuwa na uwezekano mkubwa wa kupata wawekezaji wengi.

“Wawekezaji wengi wanaenda Kenya ambayo ilipanda tangu mwaka 2015 kuliko Tanzania, tutarajie wawekezaji wengi zaidi," alisema.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umaskini (Repoa), Dk. Donald Mmari, alisema tafsiri ya hatua hiyo ni kuongezeka kwa uzalishaji katika sekta mbalimbali.

Alisema inaonyesha Pato la Taifa limeongezeka kiasi kwamba likigawanywa kwa vigezo vinavyotumika, linaiondoa Tanzania katika orodha ya nchi maskini.

“Eneo la ardhi linalolimwa limeongezeka, na uzalishaji wa mazao umeongezeka sana, sekta ya uchukuzi unaona kuna ubebabaji wa mizigo umeongezeka, sekta ya ujenzi nyumba zinajengwa na majengo mengi sana,” alibainisha.

Dk. Mmari alisema sekta ya utalii pia imeongezeka kwa idadi ya watalii kufikia zaidi ya milioni 1.5 tofauti na miaka 20 iliyopita walipokuwa 50,000 kwa mwaka.

Alisema kaya zilizounganishwa na umeme na maji zimeongezeka na wananchi wanaomiliki mali mfano pikipiki ambazo kwa sasa vijana wengi wanamudu kununua. Pia kaya zinamiliki redio, luninga na dhana za kisasa za kilimo.

Mtaalamu huyo pia alisema nyumba za bati zimeongezeka kwa sasa, tofauti na miaka 20 iliyopita ambapo nyumba nyingi ziliezekwa kwa nyasi.

“Kuna uwezekano wa mikopo nafuu kupungua kwa kuwa unapofikia pato la kati la chini, kuna misaada ulikuwa unapewa kama mikopo ambayo mingi iliangalia hatua za uchumi, utaiokosa.

"Kenya riba yao ni kubwa kidogo. Nchi maskini zinaonewa huruma kwa sababu ya pato lao. Kama mkopo riba ni asilimia 15, nchi maskini inapewa asilimia 10, kwa hatua hii tutaingia kwenye riba kubwa,” alisema.

Alisema pia fedha za misaada ambayo Tanzania ilipaswa kuzipata bure, itazikosa kwa sababu imekua kiuchumi.
Alisema kuwa, pamoja na mafanikio yaliyofikiwa, kunahitajika jitihada za zaida kuendana na ongezeko la watu, kinyume chake uchumi utasuasua.

*Imeandikwa na Augusta Njoji (DODOMA) na Salome Kitomari (DAR)

Habari Kubwa