Familia ya Mtanzania aliyeuawa kwa risasi Marekani yaomba msaada

20Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Familia ya Mtanzania aliyeuawa kwa risasi Marekani yaomba msaada

Familia ya Kijana Mtanzania Humphrey Magwira (20) aliyeuwawa kwa kupigwa risasi nchini Marekani imeomba jamaa,ndugu na marafiki kusaidia kuwezesha kusafirisha mwili wa marehemu kwenda kuzikwa nyumbani Tanzania.

Humphrey Magwira (20).

Kijana huyo alipigwa risasi siku ya Ijumaa kufuatia ajali ya gari alilokuwa akiendesha kugonga gari ndogo katika eneo la Fort Bend na kisha kushambuliwa na kijana aliyefahamika kwa jina la Ramon Vasquez (19) ambaye alikamatwa Jumamosi ya Oktoba 16 na kufunguliwa mashtaka ya mauaji.

Humphrey ambaye ni Mwanafunzi wa Uhandisi wa Kompyuta katika Chuo Kikuu cha Houston, Marekani alifikwa na mauti muda mfupi kabla ya kufikishwa hospitali baada ya kushambuliwa na risasi mfululizo katika makutano ya Barabara ya Beechnut na Addicks Clodine yaliyopo Kaunti ya Fort Bend.

Uchunguzi wa tukio uliendelea, na maafisa wa polisi walifanikiwa kumkamata  mtuhumiwa asubuhi ya Jumamosi, Oktoba 16 na kumfungulia shitaka la mauaji. Ramon bado yuko kizuizini ingawa polisi wametangaza dhamana ya kiasi cha Dola za Marekani  500,000 sawa na zaidi ya Sh bilioni 1.152. Wazazi wa marehemu wametaka haki dhidi ya Humphrey itendeke.

Kaka wa marehemu, Rodricque ameanzisha kampeni kuhamasisha watu kuchangia gharama za kusafirisha mwili wa marehemu kupitia mtandao ‘GoFundMe’ na akaunti ya simu (0715-447436- na 0754-447436) zote zimesajiriwa kwa jina la Janet Kuyangana.

Habari Kubwa