Fao upotevu wa ajira sasa ndani ya siku 14

29Apr 2019
Salome Kitomari
DAR ES SALAAM
Nipashe
Fao upotevu wa ajira sasa ndani ya siku 14
  • *880 wabainika kughushi nyaraka  kujipatia mabilioni NSSF...

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umesema ulipaji wa mafao ya ukosefu wa ajira sasa unafanyika ndani ya siku 14 iwapo mwanachama amekamilisha nyaraka zote.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Willium Erio

Vilevile, mfuko huo umesema katika ukaguzi wa nyaraka za waombaji wa fao la upotevu wa ajira kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, maombi 880 yenye madai ya Sh. bilioni 8.8 yalibainika kuwa feki.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Nipashe jijini Dar es Salaam wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Willium Erio, alisema kwa mujibu wa utaratibu, fao la upotevu wa ajira linatakiwa kutekelezwa ndani ya siku 30, lakini wameamua kurahisisha ili kuondoa usumbufu kwa wanachama.

Alibainisha kuwa katika kushughulikia madai ya miezi mitatu iliyopita, baadhi ya wanachama baada ya ufuatiliaji wa kina, walibainika wanadanganya kwamba hawako kazini, ilhali wako kazini.

“NSSF tumejiwekea utaratibu wa kulipa fao la ukosefu wa ajira ndani ya siku 14 baada ya mhusika kuwasilisha nyaraka zote muhimu, ikiwamo mwajiri kupeleka michango yote kwa wakati, lakini utaratibu wa kisheria ni siku 30,” Erio alisema.

Fao la upotevu wa ajira kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya Mwaka 2018 ni asilimia 33.3 ya mshahara wa mhusika wakati anaachishwa kazi, na inatakiwa awe ameachishwa kazi na siyo kuacha kwa hiyari.

Alisema mafaili ya waombaji waliogushi nyaraka yamekabidhiwa kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya kuwakamata na kuwafikisha mahakamani kwa udanganyifu na kughushi nyaraka.

“Kuna udanganyifu sana katika fao la upotevu wa ajira, hili ni tatizo la kitaifa ambalo litamalizwa na uwapo wa vitambulisho vya taifa kwa kuwa kila mmoja atakuwa na namba yake na taarifa zake zikiwekwa itaonyesha anafanya kazi wapi," alisema.

Erio aliongeza: “Mtu anakwambia ameachishwa kazi, lakini ukifuatilia yuko sehemu nyingine anafanya kazi, siyo kila anayeleta madai NSSF ni madai sahihi wengine wanadanganya na tunawakamata mara kwa mara."

Alisema wengi wanalalamika lakini madai yao yakichunguzwa kwa kina, inabainika si wanaostahili, lakini kwa wale wanaokutwa hawana matatizo yoyote, wanalipwa kwa wakati.

Alisema fao la upotevu wa ajira linatolewa kwa mtu mwenye taaluma ambaye ameachishwa kazi na atalipwa asilimia 33.3 ya mshahara wake, kama mbadala wa mshahara wakati anasubiri kupata kazi nyingine.

Kwa mujibu wa Erio, katika siku 23 za mwezi huu (Aprili 1-23), walilipa Sh. milioni 504.7 kwa wanachama waliodai fao hilo.

Aliongeza kuwa kuna changamoto kubwa ya wanaoachishwa kazi, akieleza kuwa mwanachama anaachishwa kazi leo, siku inayofuata anakwenda kwenye ofisi za mfuko kudai fao la upotevu wa ajira, jambo ambalo alisema siyo sahihi.

Alisema tangu mwaka jana hadi sasa, watu 15,258 wanalipwa fao la ukosefu wa ajira na Sh. bilioni 36.55 zimetumika.

Alisema kwa upande wa wanachama wasio na taaluma wanaochukua michango yao, 995 wameshalipwa, akifafanua kuwa ni wale ambao walikuwa wanafanya kazi za vibarua kwenye barabara, migodi na shambani.

WAKATI GANI KUFUATILIA MAFAO?Alisema kwa mujibu wa utaratibu, mwajiri amepewa mwezi mmoja zaidi kuwasilisha michango ya wanachama, hivyo mwanachama kuachishwa kazi mwezi huo na kwenda kudai mwezi huo huo, michango yake inakuwa bado haijaufikia mfuko, mara nyingi mchango wa mwezi wake wa mwisho kuwa kazini.

“Inatakiwa ukiachishwa kazi, ukae mwezi mmoja ndiyo uende kwenye mfuko ili mchango wako uletwe, itakuwa rahisi kupiga hesabu kwa kutumia mshahara wa mwisho mwanachama alioachishwa nao kazi,” alisema.

"Kwa mfano, michango ya mwezi wa nne itapelekwa mwezi wa tano, na malipo ya aliyepoteza ajira yataanza Juni mwaka huu.

“Mtu anataka akiachishwa kazi leo, basi kesho aje kwenye mfuko na siku inayofuata apewe fedha, utaratibu hauko hivyo maana ni lazima tupitie nyaraka na kufanya uchunguzi wa kina na baada ya kujiridhisha mhusika ataanza kulipwa kila mwezi."

Habari Kubwa