Fatma Karume amwagiwa sifa kila kona

19Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Fatma Karume amwagiwa sifa kila kona

SIKU moja baada ya Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume, kutangaza rasmi kutowania tena uongozi katika chama hicho, wadau mbalimbali wa sheria na wanachama wamemwelezea kuwa mwanamke wa kwanza alionyesha uwezo mkubwa.

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume, picha mtandao

Bob Wangwe, mtoto wa mbunge wa zamani wa Tarime, Chacha Wangwe, alisema jana kuwa kwa kipindi kifupi alichoongoza TLS ameonyesha uwezo mkubwa tofauti na ilivyodhaniwa hapo kabla.

Wangwe ambaye ni mshirika mkubwa wa mwanasheria huyo machachari, alisema:

“Fatma ni mtu ambaye ana uwezo na ameonyesha uwezo wake na uamuzi wake wa kutogombea umenisikitisha sana. Wengi tulipenda aendelee lakini sasa hatuna jinsi,” alisema Bob.

Kuhusu kauli ya kiongozi huyo kuwa mahakama inachagua watu wa kufanya nao kazi na kutopendelea kufanya kazi na wanaharakati, alisema ni pigo kwa ustawi wa mahakama na ni jambo la kusikitisha.

“Kama ni kweli basi ni pigo kubwa sana kwa ustawi wa mahakama. Ikitokea kwamba mahakama inabagua wanaharakati basi ni jambo la kusikitisha sana, tunatarajia mahakama labda ikatae kufanya kazi na wezi na wahalifu wengine lakini si wanaharakati,” alisema Bob.

Naye Wakili Jebra Kambole, ambaye ni mwanachama wa TLS, alisema Fatma alifanikiwa katika sera zake nyingi, hivyo kumfanya kuwa mmoja wa marais waliopata mafanikio katika kukiongoza chama hicho.

“Uongozi wake ulikuwa mzuri, alifanikiwa kuisemea TLS na wananchi mahali panapokuwa na mkwamo kiuhusiano, kuwasemea wafungwa na kuweka wazi msimamo wake juu ya wakuu wa mikoa na wilaya kuweka holela watu ndani,” alisema.

Fatma Karume ambaye ni mtoto wa Rais wa zamani wa Zanzibar Amani Abeid Karume, alishinda kiti cha urais wa chama hicho cha wanasheria mwaka jana, akirithi mikoba ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, baada ya kuwabwaga Godwin Mwapongo, Godfrey Wasonga na Godwin Ngwilimi.