FCS yazindua mpango mkakati wa miaka mitano

26Sep 2021
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
FCS yazindua mpango mkakati wa miaka mitano

TAASISI  ya Uwezeshaji wa Asasi za Kiraia ya Foundation for Civil Society (FCS), imezindua mpango mkakati wa miaka mitano wa utendaji kazi kuanzia wa kuanzia mwaka 2022 hadi 2026.

Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation For Civil of Society (FCS) Francis Kiwanga.

Mpango mkakati huo pamoja na mambo mengine unalenga kuimarisha utawala bora hasa kuhamasisha wananchi kushiriki shughuli za maendeleo ya Taifa, ili kuwa na Taifa linalojitegemea.

Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation For Civil of Society (FCS) Francis Kiwanga, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi huo amesema,  mpango huo unazindiwa wakati ambao wamefanikiwa kufanyakazi kwa mafanikio makubwa katika mpango kazi uliopita ambapo walifanyakazi ya kuimarisha utawala bora na kupambana na ukatili wa kijinsia nchini.

Ametaja maeneo mengine waliyofanikiwa ni kuongeza hamasa ya wananchi kushiriki katika maendeleo bila kuangalia hali ya uchumi ya mtu mmoja mmoja na kuongeza kundi la walemavu, wanawake, watoto na wazee.

"Kuzindua mpango mkakati huu maana yake tumekuja na kazi zetu za kutuongoza katika miaka mitano hasa tumeangalia vipaumbele vya Taifa katika kuelekea Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDG's)," amesisitiza.

Amesema hali halisi ya maisha ya Watanzania imewasukuma kutengeneza mpango kazi huo, utakaosaidia kwenye maeneo hayo.

Ametaja eneo lingine watakalofanyia kazi ni kuongeza kipato cha wananchi kwa kuzingatia mabadiliko ya tabia ya nchi  kuwa kuna kundi la walemavu, vijana na wanawake waliopo pembezoni ambao wanahitaji kupiga hatua.

Kiwanga amesema eneo lingine la ulinzi na amani ni muhimu kwa sababu limechukua miaka 60 msingi wake kujengwa, kazi kubwa iliyofanywa ili kuendelea kuishi na kufanya shughuli kwa amani.

"Kuna kundi la watu limejitokeza kutaka kuharibu amani ya nchi. Migogoro ya kugombea rasilimali hivyo ni lazima tujenge jamii inayoweza kutatua migogoro wenyewe na kuchukua hatua na kuendelea na shughuli zao za uchumi," amesema Kiwanga.

Amesema kwa kushirikiana na serikali, wabia wa maendeleo, asazi za kiraia na wananchi wenyewe watafanikiwa kutekeleza mpango huo kikamilifu.

Kadhalika amesema pia wanatumia Sh. bilioni 10 hadi 13 kila mwaka, katika kuhakikisha wanazifikia asasi za kiraia zaidi ya 150 kila mwaka na kwamba asilimia 90 ya rasilimali fedha hizo zinaenda kwa asasi za vijiji ambazo zipo ngazi ya mashina.

Aidha, amesema kutokana na kuwapo na mabadiliko ya tabia nchi kidunia na UVIKO-19  kutikisa dunia, wanatoa uwezeshaji kwa asasi hizo ili kuisaidia jamii kuenenda na hali iliyopo katika kutekeleza majukumu yao.

Naye Rais wa Taasisi hiyo Dk. Stigmata Tenga, amesema kuwa Asasi za Kiraia zinapaswa kujengwa kutokana kuwa ni muhimili mkubwa wa maendeleo nchini nakwamba wananchi wanapaswa kuzifahamu.

“Tuisemee sekta hii na yale yote ambayo sekta hii inayafanya kwenye jamii, yasemeeni mnayoyafanya ili yajulikane msione aibu yeyote,”amesema Dk. Tenga.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Asasi za kiraia, Dk. Richard Samabiga, ameipongeza FCS kwa hatua hiyo ya kuzindua mpango mkakati huo ambao unaonyesha dira ya kusaidia wananchi katika maeneo mbalimbali.

Amesema mpango huo unaleta matumaini makubwa kwa asasi za kiraia katika kufanya kazi zao za kusaidia wananchi.

Habari Kubwa