Fedha za Watanzania zitatumika hivi mwakani

11Jun 2021
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Fedha za Watanzania zitatumika hivi mwakani

KIASI cha Sh. trilioni 36.33 kinatarajiwa kukusanywa na kutumika na serikali kwa mwaka 2021/22, huku Sh. bilioni 328.2 zikitengwa kwa ajili ya maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.

Akiwasilisha bungeni jana mapendekezo ya bajeti ya serikali kwa mwaka huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh. trilioni 26.03, sawa na asilimia 71.7 ya bajeti yote yakiwamo yanayotokana na mapato ya kodi Sh. trilioni 22.18, sawa na asilimia 13.5 ya Pato la Taifa.

Alisema serikali inalenga kukusanya mapato yasiyo ya kodi ya Sh. trilioni 2.99 na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri Sh. bilioni 863.9.

Alisema washirika wa maendeleo wanatarajia kuchangia misaada na mikopo nafuu Sh. trilioni 2.96, sawa na asilimia 8.1 ya bajeti yote ambapo kiasi hicho kinajumuisha fedha za miradi ya maendeleo Sh. trilioni 2.67 na Mifuko ya Pamoja ya Kisekta Sh. bilioni 282.3.

Dk. Nchemba alisema serikali inatarajia kukopa Sh. trilioni 7.34 kutoka soko la ndani na nje kwa masharti ya kibiashara (Sh. trilioni 4.99 ni mikopo ya ndani ambayo inajumuisha Sh. trilioni 3.15 kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za serikali zinazoiva na Sh. trilioni 1.84 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo).

Alisema Sh. trilioni 2.35 zinatarajiwa kukopwa kutoka soko la nje kwa lengo la kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Dk. Nchemba alisema kwa upande wa mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara, serikali ipo katika hatua za mwisho za majadiliano na baadhi ya taasisi za fedha za kimataifa ili kuhakikisha kiasi kilichopangwa kukopwa kinapatikana.

Vilevile, alisema serikali itaendelea kutoa elimu kwa umma kwa lengo la kuongeza ushiriki wa wawekezaji kwenye soko la ndani la fedha ili kuhakikisha kiasi kilichopangwa kukopwa kinapatikana kwa wakati.

Akizungumzia viashiria vinavyopima uwezo wa nchi kulipa deni, alisema vinaonyesha Tanzania ina uwezo wa kuendelea kukopa kutoka ndani na nje ya nchi ili kugharamia miradi ya maendeleo na pia ina uwezo wa kulipa mikopo inayoiva kwa wakati.

MATUMIZI

Waziri huyo alisema serikali inapanga kutumia Sh. trilioni 36.33 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati yake, Sh. trilioni 23 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh. trilioni 13.33 kwa ajili ya maendeleo, sawa na asilimia 37 ya bajeti yote.

"Kati yake, Sh. trilioni 10.37 ni fedha za ndani na Sh. trilioni 2.96 za nje. Fedha za maendeleo zinajumuisha Sh. trilioni 1.19 kwa ajili ya miradi ya reli, Sh. trilioni 2.08 kwa ajili ya miradi ya barabara, ujenzi wa madaraja na viwanja vya ndege.

"Sh. trilioni 2.34 kwa ajili ya miradi ya kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme ikiwamo mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere, Sh. bilioni 589.4 kwa ajili ya miradi ya maji mijini na vijijini, Sh. bilioni 233.3 kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, Sh. bilioni 500 ni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu," alisema.

Pia, alisema Sh. bilioni 312.1 zitatumika kugharamia mpango wa elimumsingi bila ada na serikali imetenga Sh. bilioni 400 kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya miradi ya maendeleo.

Alisema Sh. trilioni 8.15 zimetengwa kwa ajili ya mishahara na Sh. trilioni 4.19 kwa ajili ya matumizi mengineyo.

Waziri huyo alisema Sh. trilioni 10.66 zitatumika katika ulipaji wa Deni la Serikali, huku Sh. bilioni 200 zikitumika kulipa madeni yaliyohakikiwa ya watumishi, wazabuni na watoa huduma.

BAJETI 2020/21

Mwaka huu, serikali ilipanga kukusanya kiasi Sh. trilioni 34.88 kutoka katika vyanzo vyote vya ndani na nje. Hadi kufikia Aprili mwaka huu, Sh. trilioni 24.53 zilikuwa zimekusanywa sawa na asilimia 86.1 ya lengo la kipindi hicho.

Alifafanua kuwa mapato yaliyokusanywa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yalifikia Sh. trilioni 14.54, sawa na asilimia 86.9, Mapato yasiyo ya Kodi yalifikia Sh. trilioni 1.8, sawa na asilimia 78.5 ya lengo.

Pia alisema mapato yanayotokana na vyanzo vya ndani vya Mamlaka za Serikali za Mitaa yalifikia Sh. bilioni 607.4 sawa na asilimia 88.5 ya lengo huku misaada na mikopo nafuu iliyopokelewa ilikuwa Sh. trilioni 1.89 sawa na asilimia 70.4 ya lengo.

Mikopo ya ndani ikijumuisha mikopo ya kulipa dhamana za serikali zilizoiva ilifikia Sh. trilioni 3.99, sawa na asilimia 95.7 ya lengo na mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara ilifikia Sh. trilioni 1.68, sawa na asilimia 88.1 ya lengo.

Waziri Nchemba alisema mlipuko wa corona umesababisha kutofikiwa kwa baadhi ya malengo ya makusanyo ya mapato ya ndani hususan kwa sekta za utalii, usafiri wa anga na uingizaji wa bidhaa kutoka nje.

Pamoja na athari za mlipuko wa ugonjwa huo, waziri huyo alisema misaada na mikopo nafuu iliongezeka kwa asilimia 3.84 kulinganishwa na kiasi kilichopokewa katika kipindi kama hicho mwaka 2019/20.

Habari Kubwa