Fidia inavyouweka njia panda uchimbaji wa graphite Ulanga

13Feb 2020
Salome Kitomari
DAR
Nipashe
Fidia inavyouweka njia panda uchimbaji wa graphite Ulanga
  • *Wakazi wako tayari kuondoka, mtihani 'chao'
  • *Miezi 27 wawekezaji hawajui mwanzo lini
  • *Mwenyekiti Halmashauri alia kutelekezwa

BADO ni kitendawili ni namna gani utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa madini ya kinywe au graphite wilayani Ulanga mkoani Morogoro, kikisimama katika njia panda; uanze vipi na uendelee vipi?

WAZIRI WA MADINI DOTTO BITEKO.

Wakati serikali kwa upande wake imeshatoa ruksa kwa mradi huo kuanza, upande wa pili wa sarafu, nyenzo kuu inayowezesha mradi kuanza msamiati wa 'fidia' bado haujatekelezwa kuwafanya wakazi na wawekezaji wengine wa huduma za umma kama vile kanisa, kupisha eneo wakiwa na rasilimali za kuanza maisha kwingineko.

Kimsingi, huo si uamuzi wa hiari tu au makubaliano chini ya mwembe wa halmashauri fulani, bali ni mwongozo rasmi ya sheria, tena unaoenda mbali zaidi, ukitoa kipindi maalum cha malipo kufanyika kwa miezi 24 liwe limeshatekelezwa.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga, Nasoro Kihiyo, sheria inatamka kuwa ni miaka miwili fidia iwe imekwishalipwa na baada ya hapo ni lazima kufanyike hesabu mpya kutathmini gharama za kucheleweshana.

Kihiyo anasema tarehe hiyo ya kuanza kufanyiana hesabu mpya na gharama za ziada, ilishatimu wastani wa miezi mitatu sasa au kwa usahihi zaidi, Novemba mwaka jana.

HALI IKOJE?

Kampuni tatu zimeshapata vibali vya kuchimba madini ya kinywe kutoka Wizara ya Madini, lakini hazijaanza kazi hiyo kutokana na sababu mbalimbli, moja ya kampunji hizo ikiwa imefanya tathmini miaka mitano iliyopita.

Kampuni hizo ni Mahenge Resource, Kibarani na Tanzania Graphite ambazo zimepewa kibali cha kuchimba madini hayo katika maeneo ya Nawenge, Msogezi, Epanko, Mdindo, Liandu, Msogezi na Kisewe.

Kampuni ya Tans Graphite ilianza taratibu tathimini tangu mwaka 2015, lakini hadi sasa imeshindwa kulipa fidia kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni mabadiliko ya Sheria ya Madini yaliyofanyika mwaka 2017 yaliyoilazimu isimamishe ulipaji wa fidia.

Tans Graphite ni kampuni tanzu ya kampuni ya Kibaran Resources Limited yenye makao makuu yake Australia ikiwa na maeneo matano ya uchimbaji madini, ambayo ni Mirerani (maeneo mawili), Tanga na Mehenge inakochimba graphite.

Katika tovuti ya Kampuni ya Kibaran Rerources, inaelezwa kuwa Kampuni ya Tans Graphite ilifanya utafiti mwaka 2012/13 na kubaini kuwapo kwa wingi kwa madini ya kinywe nchini.

Januari 2014, kampuni hiyo ilifanya tathimini ya mazingira katika eneo la Merarani, Arusha na ilipata leseni mwaka 2015 kwa ajili ya kuanza uchimbaji.

Kampuni hiyo inaeleza kuwa madini hayo yatauzwa Ujerumani na nchi zingine za Bara la Ulaya zenye viwanda vya chuma, huku ikibainisha kuwa masoko ya madini hayo pia yako Marekani, Asia, Japani na Korea Kusini.

Katika tovuti ya Tanzania Invest, inaelezwa kuwa mwaka 2014, China ilikuwa mzalishaji mkubwa wa madini hayo ikiwa na tani 780,000, ikifuatwa na India tani 170,000, Brazil tani 80,000 na kwamba Tanzania itakuwa nchi yenye uzalishaji mkubwa wa madini hayo.

Diwani wa Nawenge, Protas Lunkombe, ambaye ni mmoja wa wanaotakiwa kufidiwa kupisha mradi huo, anasema wananchi wa Kijiji cha Epanko wanatakiwa kupisha eneo hilo na muda wa uthamini ulishaisha, lakini kampuni zimechelewa malipo ya fidia.

“Mara kadhaa tumeuliza wanasema uthamini hautaanza upya, bali watafanya malipo kabla muda haujapita sana. Wananchi wameshindwa kufanya maendeleo yoyote kwa kuwa wamezuiwa na hawajui lini watalipwa.

“Hakuna chochote kanachondelea, mtu anaogopa kufanya chochote, kadri wanavyozidi kuchelewa, ndivyo nasi tunazidi kukwama," analalamika.

JUHUDI ZA MBUNGE

Jukumu la msingi la mbunge ni kutetea maslahi ya wananchi anaowawakilisha. Mbunge wa Ulanga Mashariki, Goodluck Mlinga, anasema sheria za madini zilizopitishwa miaka ya karibuni zimekuwa kikwazo kwa kampuni zilizokuwa zimefanya tathmini ya fidia katika mradi huo.

“Kuna wawekezaji wengi wamekwama kutokana na sheria mpya zilizopita, rasilimali zao na fedha walizokopa haziwiani," anasema.

Mbunge huyo anasema Kampuni ya Tanzania Graphite ilipaswa kulipa fidia mwishoni mwa mwaka jana, lakini haijafanya hivyo kutokana mabadiliko ya kisheria, hususani kwenye masuala ya kibenki.

Mlinga anasema uthamini wa kwanza umekufa na wanatakiwa wafanye makadirio kulingana na bei ya soko la sasa, lakini hakuna kilichofanyika.

“Kampuni ya Mahenge Resource wanahamasisha wananchi ili kufanya uthamini wa waliokuwa wameufanya awali, Tanzania Grahite wameshindwa kulipa kama walivyopaswa kufanya hivyo ndani ya miaka miwili," anasema.

Mbunge huyo pia anaeleza kuwa wapo wananchi waliokuwa wamekataa fidia, likiwamo Kanisa Katoliki Jimbo la Mahenge na mpaka sasa utatuzi wa tatizo hilo bado haujafanyika ipasavyo.

“Kanisa bado hawajafikia mwafaka mzuri kwa kuwa walitaka watafute mtu wao wa mthamini, eneo likishakuwa na soko au kanisa thamani inapanda, lakini wathamini walichukua kama mashamba,”anasema.

Mbunge huyo anasema kuwa familia 52 na vikundi mbalimbali vya kijamii vilikuwa vimekataa uthamini wa awali, lakini idadi yao imeendelea kupungua.

“Wananchi wamekaa muda mrefu bila kulipwa, kwa mahesabu ya kawaida ni miaka mitano sasa wananchi wanashindwa kuendeleza maeneo yao.

“Nazungumza na serikali, kuna vitu vingi havijakaa sawa, suala la hisa kwenye migodi mikubwa, mambo mengi yamekwama, wananchi wanapata tabu hasa wa Epanko, wanasubiri vitu ambavyo hawajui lini vitawezekana au watafidiwa na kuondoka," anasema.

KAULI YA ASKOFU

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mahenge, Agapitus Ndorobo, anasema kanisa linamiliki ardhi katika maeneo ya Mdindo, Liandu, Epanko, Msogezi na Kisewe ambako kote kuna madini hayo.

Anasema kwa miaka mitano sasa, kanisa limeshindwa kufanya maendeleo yoyote katika eneo la Epanko kutokana na kusubiri taratibu mbalimbali kufanyika.

Askofu huyo alibainisha kuwa awali kanisa lilitaka kuwa na ubia na kampuni zinazokwenda eneo hilo na siyo kulipwa fidia, lakini baada ya tafakuri na kuona ambavyo watakapaswa kuwa na fedha nyingi za kuwekeza, wamekubali kulipwa fidia na kupisha mradi huo.

“Miaka mitano Tanzania Ghraphite hawajafanya lolote, tulishawaeleza watufidie, wakati wanataka kuchukua ardhi tutajua na hadi sasa hatujajua lolote, tunamilikia maeneo hayo tangu mwaka 1921, kuna mipangilio mingi tumekuwa nayo na lazima wafidie kulingana na hayo mazingira na soko.

“Kama wangekuwa na fedha wangelipa, walikuja Mahenge Resource, nikawaambia kama wanaingia kazini, lazima wawasiliane na kanisa, baadaye nimeaambiwa wamefanya utafiti hadi maeneo ya kazini.“Kama kanisa, tunataka watulipe na tutasema tunahama kila mahali, lazima tuwaze kuwa na ubia maana ardhi ni yetu na kila mahali sasa watatuhamisha.

“Madini yapo lakini kampuni zinaweza kuchimba, na je wamefidia? Tanzania Ghraphite wamejenga nyumba mbili za mfano eneo la Epanko, lakini hadi sasa hawajaja kanisani kufanya mazungumzo kwamba watatulipaje," anasema.

Askofu huyo anabainisha kuwa upo uwezekano mkubwa wa athari za kimazingira hasa kwenye maji, kwa kuwa uchimbaji utafanyika milimani na wananchi wanategemea maji kutoka kwenye milima hiyo.

“Katika hili, tunataka mazungumzo kwa kuwa maji haya yanakwenda hadi Mto Kilombero, unaotegemewa na mamilioni ya wananchi kwa ajili ya chakula, kunywa na shughuli za kilimo. Tunataka kujua ni kwa kiasi gani maji hayataharibika,” anasema.

KIINI CHA TATIZO

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga, Kihiyo, anasema kwa mujibu wa sheria tathmini inapofanyika, inatakiwa wahusika walipwe fidia ndani ya miaka miwili, na inapopita wahusika wanapaswa kulipwa gharama za usumbufu na tathimini kufanyika upya.

Anasema kwa Kampuni ya Tanzania Graphite inayowekeza katika Kijiji cha Epanko, muda wa kulipa fidia uliisha Novemba mwaka jana, na iliahidi kulipa fedha za usumbufu ili ifanye uthamini upya, lakini hadi sasa ukimya umetawala.

Kihiyo anasema kampuni hiyo imejenga nyumba za mfano kwenye kaya mbili ambazo zimeshawishi wananchi wengi kukubali fidia na kuachana na msimamo wa awali.

“Kampuni hiyo ilijenga nyumba mbili za mfano za matofali ambazo kwa hadhi ya kijijini, ilileta mabadiliko makubwa na wananchi wengi wamejikuta wanapenda kujengewa nyumba kama hizo,” anasema.

Kihiyo anasema mabadiliko ya sheria ya madini yaliyotaka serikali iwe na hisa asilimia 16 kwenye kila mgodi, yaliwafanya wawekezaji washindwe kusonga mbele kwa kuwa hawakuwa na uhakika na usalama wa uwekezaji wao.

Kihiyo anasema kitendo cha serikali kuingia makubaliano na Kampuni ya Barrick hivi karibuni, kimetoa mwongozo wa namna mgawanyo wa hisa unavyopaswa kuwa.

“Tathimini ikishafanyika, kazi zinasimama, wananchi wameshindwa kufanya maendeleo yoyote kwa miaka miwili wakisubiri kulipwa fidia, lakini sheria inasema ukishafanyiwa tathimini, miaka miwili ikipita, wanatakiwa kuanza upya, na ili wapewe kibali cha tathimini nyingine, lazima waonyeshe ushahidi wa fedha za kulipa ili wasisumbue watu,” anasema.

Kihiyo alisema halmashauri hiyo ilianishwa mwaka 1984, lakini tangu wakati huo, haijawahi kupata hata senti moja kutokana na uchimbaji wa madini hayo, matarajio yakiwa ni kunufaika na asilimia 0.3 ya mauzo kisheria.

“Tunataraji kupata asilimia 0.3 inayotokana na mauzo ya migodi yote, mfano wakiuza vipande 1,000, sisi tunachukua vitatu, matarajio kama migodi yote mitatu itaanza uzalishaji, tutapata Sh. bilioni moja hadi mbili kwa mwaka kwa mujibu wa bei ya madini kwenye soko la dunia,” anasema.

Kwa mujibu wa Kihiyo, uchimbaji wa madini hayo, ukianza rasmi, utaleta maendeleo makubwa wilayani humo, ikiwa ni pamoja na kuongeza mzunguko wa fedha, kuboresha miundombinu ya barabara ambazo zitaboreshwa ili kupitisha magari makubwa zaidi ya 30,000.

*ITAENDELEA KESHO

 

Habari Kubwa