Fidia inavyouweka njia panda uchimbaji wa graphite Ulanga-2

14Feb 2020
Salome Kitomari
DAR
Nipashe
Fidia inavyouweka njia panda uchimbaji wa graphite Ulanga-2
  • *Waziri: Kuwajibikia jamii lazima
  • *Mwekezaji: Shule, zahanati... zaja

SEHEMU ya kwanza ya ripoti hii jana, ilieleza mkanganyiko uliojitokeza katika vipengele vinavyowezesha mradi wa kuwekeza kwenye uchimbaji wa madini ya graphite, ukikwamishwa na kutotekelezwa kwa mahitaji muhimu ya kisheria, ikiwamo fidia.

waziri wa madini, doto biteko.

Fuatilia sehemu ya mwisho, inayojumuisha ufafanuzi kutoka kwa wahusika wakuu:

Maria Mwenti, Diwani wa Uponela, anasema katika eneo lake kuna vijiji viwili, kimoja kikiitwa Lyandu ambacho kilibainika kuwa na madini hayo katika utafiti uliofanyika miaka minne iliyopita.

“Wametueleza kuwa kuna madini mengi ambayo mchakato wa kuyatoa umeanza, ila bado hatujaelewa maana kitongoji ambako madini yamegundulika ndiko kwenye miundombinu yote ya zahanati, shule na kanisa.

“Vitongoji vingine vimetawanyika sana na wakisema huduma hizo waziondoe ziende kwingine, watakuwa wamevuruga mpangilio wetu, hadi sasa hatujui mikataba ikoje zaidi ya kuelezwa kuwa wana leseni na mikataba yote muhimu.

“Tunachotarajia ni kuwa kampuni itakayowekeza, ilete mabadiliko makubwa kwenye kata yetu ili tuone manufaa na siyo utajiri utoke ardhini halafu sisi tuendelee kuwa maskini na tukose huduma muhimu.

“Tunatamani kuona tunajengewe shule, zahanati na kituo cha afya cha kata. Tunaona wanaendelea na kazi zao za tathmini, lakini hatushirikishwi kujua kinachoendelea, mimi kama mwakilishi wa wananchi nilitarajia nishirikishwe,” analalamika.

Neema Lyafwila, mkazi wa eneo hilo, anasema kwa muda ambao wameishi bila kupata fidia, wameshindwa kufanya shughuli za maendeleo.

UFAFANUZI KISHERIA

Wakili wa Kijitegemea, Harold Sugusia, anasema kuna sheria tatu ambazo zinaguswa na suala hilo ambazo ni Sheria ya Ardhi, Sheria ya Madini na Sheria ya Uwekezaji.

Anasema Sheria ya Ardhi inasema ikitokea kuna mgongano wa kisheria katika masuala ya ardhi, sheria hiyo (Sheria ya Ardhi) ndiyo itatawala na kama kuna hizo sheria nyingine, kitakachopaswa kuangaliwa ni utaratibu wa Sheria ya Ardhi kuhusu fidia.

“Inasema kama mtu alikuwa anamimili eneo lake, likachukuliwa kwa faida ya umma, atalipwa kwa bei ya soko, kama walifanywa tathmini na ikafanywa na mtaalamu wa tathmini na ripoti ikitoka, ndiyo watu wajipange kwa ajili ya kulipwa fidia,” anasema.

Kwa mujibu wa Wakili Sugusia, madini yote yaliyo chini ya ardhi ni mali ya serikali na wananchi wanapaswa kulipwa fidia kabla ya kuanza uchimbaji.

Anasema kama tathmini ya awali ilifanyika muda mrefu na bei ya soko na hali ya maisha imebadilika, inabidi kuangalia kama ardhi imeongezeka thamani kwa kiwango gani, ili muda ukiisha walipwe kwa bei ya soko kwa wakati wanaondoka.

KAULI YA TRANS GRAPHITE

Meneja Uhusiano wa Jamii wa Kampuni ya Tans Graphite, Benard Mihayo, anasema vitongoji vitatu kati ya sita katika Kijiji cha Epanko ndiyo vitahamishwa na kwamba huduma zote muhimu za kijamii zitawekwa.

Anasema walipata leseni mwaka 2015, lakini wameshindwa kuanza kazi kutokana na mabadiliko ya Sheria ya Madini, ambayo yalilazimu kampuni kujipanga upya na kuna mambo wanajadiliana na serikali kabla ya kuanza uchimbaji.

“Tumeunda kamati tisa ambazo zimewakilisha makundi yote kwenye jamii, hadi sasa asilimia 82 ya wananchi wamekubali kulipwa fidia ambayo itaanza kulipwa baada ya kampuni kukubaliana na serikali,” anasema.

Mihayo anaendelea kueleza kuwa mwekezaji huyo anatarajia kuwekeza zaidi ya Sh. bilioni 3.7 na kati yake Sh. bilioni mbili ni za ujenzi wa nyumba za kisasa za wananchi hao.

“Tumetengeneza mpango wa maendeleo wa miaka miwili baada ya kuwajengea wananchi nyumba za kisasa katika eneo tutakalowahamishia, tutawapa mbolea na pembejeo zote muhimu kwa ajili ya kuboresha ardhi mpya watakayokwenda kuitumia,” anaahidi.

Anasema kwa mujibu wa sheria, walipaswa baada ya kutangaza kulipa fidia, kufanya hivyo lakini ikipita miezi sita bila kulipa, watatakiwa kulipa pamoja na faini ya asilimia sita.

Anasema walipanga kuanzia Januari mwaka jana, kujenga nyumba 350 kwa ajili ya wananchi wanaohama kupisha mradi. Kwa upande wa huduma za kijamii, anasema wamepanga kujenga Shule ya Msingi Epanko yenye madarasa 14 ikiwamo darasa la awali ambayo itabeba wanafunzi 332.

Pia anasema watajenga zahanati ya kisasa, kituo cha afya na nyumba tatu za madaktari, ofisi za kijiji na miundombinu ya barabara ya kuingia na kutoka kwenye eneo la mradi.

Anabainisha kuwa leseni waliyopewa ni ya miaka 12 na wanaruhusiwa kuihuisha na kwamba watakuwa wanalipa mrabaha wa asilimia 0.3 kwa halmashauri.

WAZIRI ANENA

Hivi karibuni akizungumza na wananchi wa Mahenge, Waziri wa Madini, Dotto Biteko, alizitaka kampuni zote zinazowekeza kwenye sekta ya madini, kutekeleza ahadi ya uwekezaji kwenye huduma za jamii kama walivyoahidi wakati wanaomba leseni.

"Niwatoe wasiwasi wananchi kuwa hakuna mtu hata mmoja atakayekuja Tanzania kuchimba madini, aondoke na kuwaacha wananchi wanashangaa, zama hizo zilipendwa.

"Wawekezaji wote watakaokuja, watachimba na madini watakayoyapata faida yake lazima irudi Tanzania," alisisitiza.

Waziri Biteko pia alisema soko la madini ambalo limeanzishwa Aprili mwaka jana Ulanga, limewezesha serikali kupata mapato, akibainisha kuwa hadi sasa, fedha iliyopatikana kutokana na mauzo ya madini hayo ni Sh. milioni 396 wakati kwa miaka mitano iliyopita walipata Sh. milioni nne tu.

Alisema matarajio ya wizara yake ni mapato kuongezeka zaidi pale wawekezaji hao watapoanza kazi rasmi.

Akizungumzia Kampuni ya Mahenge Resources, Waziri Biteko alisema: “Uwekezaji wao ni wa Dola za Marekani milioni 23 zitakazojenga mgodi huo wa Mahenge Resources. Kikwazo walichonacho ni fidia kwa wananchi, tayari tumeshawaelekeza waikamilishe haraka kabla ya uwekezaji, wameomba katika mchakato huu timu ya uthamini iwe na wawakilishi.

“Tayari nimemwelekeza Mkuu wa Wilaya wa hapa, wawe na wawakilishi wa kijiji kwenye timu hiyo ili baadaye kusitokee malalamiko.”

Waziri Biteko alisema kampuni hiyo imeshapewa sampuli mbalimbali za madini hayo ambazo walizipeleka katika maabara tofauti na wamejiridhisha, kinywe ya Tanzania ni bora kuliko zinazopatikana maeneo mengine duniani.

 

GRAPHITE NI NINI?

Mtaalamu wa miamba kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Hudson Nkotagu, anasema madini ya graphite kwa Kiswahili yanafahamika kama grafiti na yanapatikana katika ukanda ambao kitaalamu wanauita ‘Mozambican Belt’, unaotokea Ethiopia na kupitia katika nchi za Afrika Mashariki hadi Msumbiji.

“Mara nyingi ukanda huo una miamba yenye umri wa zaidi ya miaka bilioni 1.2 ‘metamophic’, ambazo zina joto la chini, kati na juu sana.

"Miamba ambayo imetengenezwa kwenye joto la chini ndiyo inaweza kuwa na hiyo miamba yenye madini ya graphite ambayo ni kama viumbe hao kama mimea ambayo hupikwa kwenye joto la chini na kutengeneza madini hayo,” anasema.

Anaeleza kuwa madini hayo kwa Tanzania yako Mirerani mkoani Arusha, Mahenge mkoani Morogoro na Ngachu mkoani Lindi, ambako wanakuita Ukanda wa Usagarani.

Prof. Nkotagu anasema graphite ni madini yenye nguvu kwa kiwango kikubwa kupita malighafi nyingine yoyote duniani, yakifananishwa na chuma cha pua mara 200.

“Hiyo sifa inayafanya yaweze kutumika kwenye vitu vingi kama kutengeneza madaraja, bodi za ndege, gari, kofia za pikipiki na vitu vingine vigumu vigumu. Pia yanaweza kuvutika sana kwa asilimia 20 hadi 25 ya urefu wake,” anafafanua.

Anaongeza kuwa sifa nyingine ni membamba na kwamba ukichukua gramu moja, unaweza kufunika uwanja wa mipira wa miguu (kapeti, na ni mepesi kuliko unywea wa kuku.

Anasema madini hayo yana uwezo wa kusafirisha joto kuliko vitu vingi duniani, yanasafirisha umeme kuliko hata nyaya za kopa na ndiyo maana kwenye kila kinu, kuna kidogo kimewekwa ili umeme uweze kupita kwa haraka.

“Ndiyo maana wanatumia kwenye ndege, ndege inahitaji vitu kama hivyo kwa kuwa vinaweza kupitisha umeme kwa haraka sana,” anafafanua.

Anaongeza kuwa graphite inaweza kuchuja maji na kuondoa madini mengine yote na ina uwezo wa kuyachuja maji ya bahari yakawa maji ya kunywa.

“Madini hayo yanatengeneza betri za magari na magari aina ya Voxwagon na Mercedes Benz na BMW wanataka miaka 2020/25 asilimia 25 ya magari wanayotengeneza duniani, yawe ya umeme wa kutumia graphite," anasema.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanaisukuma dunia kusaka mbinu za kupunguza hewa ukaa, yatayasukuma mataifa mengi kunaanza kutengeneza magari ya umeme na graphite itahusika kwa kiasi kikubwa kupitisha na kuhifadhi umeme kwa muda mrefu.

Anajata sifa nyingine kuwa ni kutumika kutengenezea breki za magari, kwenye chuma cha pua, kutumika viwandani kwa ajili ya vilainishi mbalimbali na kwamba ina soko kubwa duniani.

GRAPHITE YA TANZANIA

Profesa Nkotagu anasema nchi inayoongoza kwa kuwa na grafiti nyingi ni Uturuki ambayo mwaka 2017 ilikuwa na Metric tani milioni 90, ikifuatwa na Brazil yenye ikiwa na Metric tani milioni 70, China tani milioni 55 huku Tanzania na Msumbiji zikiwa na tani milioni 17.

“Grafiti ya Tanzania ni asili na yenye ubora kwa asilimia 99, katika kuchakata, uchafu ni kidogo, Ukilinganisha na wengine, ya Tanzania ni namba moja kwa kuwa ina ubora wa hali ya juu," anasema.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, nchi za Marekani na China ndiyo wanunuzi wakubwa kutokana na utengenezaji wa ndege.

Habari Kubwa