Fisi wavamia na kujeruhi msibani

23Oct 2019
Ahmed Makongo
Bunda
Nipashe
Fisi wavamia na kujeruhi msibani

WATU wawili wamenusurika kifo baada ya kushambuliwa na fisi wasiojulikana idadi yao kuvamia kwenye nyumba iliyokuwa na msiba katika kijiji cha Kasahunga Bunda, mkoani Mara.

Daktari wa Hospitali ya Misheni Kibara, Samuel Paul, alithibitisha kupokea majeruhi David Robert ambaye amelazwa kutokana na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili ikiwamo mikono yake.

Naye muuguzi mmoja wa kituo cha afya Kasahunga, aliyefahamika kwa jina la Happy, aalisema majeruhi mwingine Elizabeth mgeta (60) amelazwa kutokana na kujeruhiwa mkono mmoja.

Mashuda wa tukio hilo, walisema fisi hao walivamia majira ya saa 6:00 usiku wa kuamkia jana.

Walisema fisi hao walivamia msibani hapo na kuanza kushambulia waombolezaji hao waliokuwa wamekaa nje wakisubiri kulala, baada ya ibada kuisha.

"Tulipomaliza ibada tulitaka kulala, fisi walivamia katika eneo hilo na kujeruhi wenzetu," alisema shuhuda mmoja.

Katika hatua nyingine, wavuvi wanne wamepoteza maisha baada ya kufa maji kutokana na mtumbi waliokuwa wanavulia samaki kutoboka na kuzama katika Ziwa Victoria, eneo la mwalo wa Kibara, wilayani Bunda mkoani Mara.

Kwa mujibu wa polisi, mvuvi mmoja Doto Mufungo (18) mkazi wa kijiji cha Kenkombyo, alinusurika kifo baada ya kushikilia mtumbwi huo na kupiga kelele za kuomba msaada na hatimaye wananchi kufika na kumwokoa.

Wavuvi waliokufa maji wametambuliwa kuwa ni Kabenjulilo Magere (17), Godluck Yohana (15), Kaitila Julius (19) na Philipo James (17) ambaye alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kenkombyo, aliyefaulu mtihani wa darasa la saba mwaka huu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo usiku wa kuamkia jana majira ya saa 7:30 usiku.
Hadi jana, mchana miili ya wavuvi wote wanne ilikuwa imepatikana na kukabidhiwa kwa ndugu zao kwa ajili ya mazishi.

Daktari wa Hospitali ya Misheni Kibara, Dk. Samuel Paul, na muuguzi Nurie Mabele, walithibitisha wavuvi hao kufa maji.

Habari Kubwa