F.M Abri yatoa vifaa kinga kwa Umoja wa Daladala Manispaa ya Iringa

22May 2020
Dotto Lameck
Iringa
Nipashe
F.M Abri yatoa vifaa kinga kwa Umoja wa Daladala Manispaa ya Iringa

KAMPUNI ya F.M Abri ya mkoani Iringa inayojishughulisha na sekta ya usafiri wa mizigo na vituo vya mafuta imekabidhi ndoo maalum 30 za kunawia na sabuni zaidi ya 100 za kutakasia mikono kwa Chama cha Madereva daladala Manispaa ya Iringa kwa lengo la kuwasaidia kupambana na ugonjwa wa corona.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa FM Abri, Arifu Abri mwakilishi wa kampuni hiyo, Yusuph Majaliwa amesema lengo la kampuni hiyo ni kuunga mkono jihudi za serikali katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Amesema kuwa msaada huo umekuja baada ya Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva Daladala Manispaa ya Iringa, Ambakisye Mwangomba kuomba msaada huo hivyo wamekabidhi msaada wa ndoo maalum za kunawia mikono pamoja na sabuni za kutakasa mikono.

Majaliwa amesema kuwa katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona ni muhimu kwa jamii kuungana na kuunga mkono serikali ya awamu ya tano katika kudhibiti janga hili janga hili ambalo limeikumba dunia na misaada kama hii inahitajika hasa kwenye huduma za usafiri.

Aidha, amesema kuwa kampuni hiyo imeendelea kusaidia jamii za mijini na vijijini kwenye mapambano dhidi ya kuenea kwa virusi vya corona kwa kutoa misaada mbalimbali na kutoa elimu kwa jamii.

Pia amesema kuwa huo ni utaratibu wa kampuni ambao umewekwa ni kwa ajili ya kusaidia jamii na kurudisha faida kwa jamii ambayo imekuwa ikiwaunga mkono katika shughuli za kila siku.

“Lengo la kampuni ni kuunga mkono serikali katika mapambano dhidi ya kuenea kwa virusi vya corona hivyo ni muhimu kutoa misaada kwa jamii yenye uhitaji hasa watu wanaohudumia watu kwa wakati mmoja ikiwemo sekta ya usafiri ambayo imekuwa ikihudumia jamii kubwa.” Amesema Majaliwa.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Daladala Manispaa ya Iringa, Clement Duma, ameipongeza kampuni ya F.M Abri kwa kuwa mstari wa mbele katika kusaidia jamii na msaada huo umekuja katika wakati mwafaka na vifaa hivyo vitasaidia mapambano dhidi ya corona.

Duma amesema kuwa watahakikisha msaada huo wanatumia ipasavyo kwa kutoa elimu kwa abiria kuweza kunawa mikono na kutoa wito kwa vyombo vya habari kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuzingatia maelekezo wanayopatiwa na wataalam wa afya kuweza kujinga dhidi ya maambukizi

Habari Kubwa