Fursa pembejeo bure wazee miaka 60

13Jan 2020
Shaban Njia
Kahama
Nipashe
Fursa pembejeo bure wazee miaka 60

WAZEE wenye umri wa miaka 60 na kuendelea katika kijiji cha Wisolele Kata ya Segese Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga, wamepatiwa zana za kilimo na pembejeo bure kwa ajili ya maandalizi ya kilimo.

Pembejeo hizo zinatolewa na uongozi wa mgodi mdogo wa pamoja Gold Mining Rush.

Akikabidhi vifaa hivyo jana, Mwenyekiti wa Mgodi huo, Hamisi Mabubu, kwa wazee 60 wanaozunguka mgodi, alisema wazee wengi katika kijiji cha Wisolele wanashindwa kulima mashamba kutokana na changamoto ya pembejeo na zana za kilimo.

Alisema kuwa ugawaji wa zana za kilimo na pembejeo utakuwa unafanyika kila mwaka hasa kwa wazee wenye umri wa kuanzia miaka 60, na kwamba kila mzee aliyepatiwa pembejeo ahakikishe analima na sio kuuza.

Pembejeo hizo ni majembe, mbegu za mahindi ikiwamo mbegu za alizeti, mbolea za kukuzia na kupandia vyote vikiwa vimegharimu kiasi cha Sh. milioni 1.5.

“Wazee wetu wana maeneo makubwa ya kilimo, lakini hawana uwezo wa kununua zana za kilimo na pembejeo, na sisi kama viongozi wa mgodi tumeliona hili na kuchukua maamuzi ya kugawa pembejeo, mbegu na zana za kilimo bure kwa wazee wanaozunguka mgodi,” alisema.

Lucas Shija, mzee wa kijiji cha Wisolele, alishukuru uongozi wa mgodi kuwapatia pembejeo na zana za kilimo bure na kudai kuwa alikuwa ameshakata tamaa ya kuendelea kulima maeneo yake baada ya kukosa pembejeo za kilimo.

Habari Kubwa